BAADA ya kupokea kichapo cha bao 1-0 kutoka kwa Wanamsimbazi, Kipa wa Yanga SC Raia wa Kenya Farouk Shikalo, amesema kuwa wao kama timu mipango yao ni katika msimu ujao kwani wamejipanga kuja kivingine mara baada ya msimu huo kuanza.
Shikalo mwenye uraia wa Kenya kwa sasa ndiye kipa namba moja wa Yanga ambapo amepata nafasi ya kucheza katika michezo ya mwisho baada ya Metacha kusimamishwa kuitumikia klabu hiyo, huku Ramadhani Kabwili akiwa chaguo la pili ndani ya Yanga.
Akizungumzia mipango yao, Shikalo amesema kuwa kitu wanachokipa nafasi kubwa kwa sasa ni mipango ya kuelekea msimu ujao kwa ajili ya mchezo wa ngao ya Jamii na mashindano ya kimataifa.
“Malengo yetu kwa sasa ni kuhakikisaha tunafanya vizuri msimu ujao kwa kuwa msimu huu umeisha na hatujafikia malengo yetu.
“Tunajipanga katika mashindano ya kimataifa yaliyopo mbele yetu hivi karibuni pia, tutahakikisha tunarekebisha makosa ya msimu huu na kuchukua ubingwa kwenye mchezo wa Ngao ya Jamii pamoja na mashindano ya Cecafa,” amesema Shikalo.