KLABU ya Moghreb Tétouan anayoichezea Mtanzania Shaaban Chilunda imeshuka daraja jana usiku baada ya kupokea kichapo cha 3-2 dhidi ya RS Berkane kwenye Ligi Kuu ya nchini Morocco.
Chilunda amejiunga na timu hiyo msimu huu lakini ameifungia mabao mawili tu na kushindwa kuisaidia kuhakikisha wanabaki kwenye Ligi Kuu ya Morocco inayofahamika kwa jina la Botola.
Moghreb inashika nafasi ya pili kutoka mwisho (15) wakiwa wamecheza mechi 30 wameshinda sita, sare 14 na wamefungwa mechi kumi hali iliyowafanya washuke daraja.
Mchezaji mwingie wa Tanzania ambaye alisajiliwa na timu hiyo ni Edward Maka lakini hajawa sehemu kubwa ya kikosi cha kwanza na mara kwa mara anaonekana akiwa nchini.
Bingwa wa Ligi hiyo ni Wydad baada ya kujikusanyia pointi 64 kwenye mechi 29 akiwa na mchezo mmoja mkononi huku nafasi ya pili ikishikiliwa na Raja Casablanca wakiwa na pointi 56 wakicheza mechi 29 na faida ya mchezo moja mkononi ambao hata wakishinda hawawezi kuifikia Wydad.