Home Yanga SC KOCHA AS VITA AFUNGUKA DILI LA MAYELE KUTUA YANGA

KOCHA AS VITA AFUNGUKA DILI LA MAYELE KUTUA YANGA


KOCHA wa muda wa AS Vita, Raul Shungu ametamka kutoka moyoni kwamba kama Yanga ikikamilisha dili la Fiston Mayele na Heritier Makambo hapatatosha kwenye Ligi Kuu Bara.

Shungu ambaye ni Mkongomani na kocha wa zamani wa Yanga, aliweka wazi kwamba hajafurahishwa kuachana na Mayele, lakini hana namna kwa vile pesa ndiyo kila kitu kwa mchezaji.

Kocha huyo alisema anayajua vizuri machachari ya Makambo na Fiston, ndiyo maana anaamini kwamba wakiungana kwa pamoja ndani ya Yanga msimu ujao kikosi hicho kitakuwa moto zaidi ya ilivyo sasa kwa vile ni watu wa kazi na hawataki masihara.

Alienda mbali zaidi kwa kukejeli timu pinzani kwamba “lazima watu wanunue mabeki.”

Shungu ambaye kwa sasa ndiye anayeziba kwa muda nafasi ya bosi wake wa zamani, Florent Ibenge aliyetimkia Morocco ameliambia Mwanaspoti kwamba anaumia kila dakika akisikia kwamba Mayele ambaye ni mfungaji bora katika timu yao anataka kutimkia Yanga.

“Fiston (Mayele) mwenyewe amenifuata na ameniambia kwamba anataka kwenda Yanga, unajua Yanga wako ndugu zangu nawapenda sana ila naumia kwamba timu yangu Vita inapoteza mtu mwingine bora kama ilivyokuwa Mukoko (Tonombe), unakumbuka nilikwambia kwamba Mukoko anajua sana.

“Kuna muda soka ni biashara, najua Vita watapata pesa kwa kuwa Mayele ni mchezaji bora na anajua kazi yake ya kufunga, Yanga wamepata mshambuliaji bora aliyekomaa kwa kujua kazi yake, unaona hapa amefunga zaidi ya mabao 13 msimu huu, hii ni ishara kwamba anaweza kushindana,” alisema Shungu.

Timu ya Horoya juzi ilimuaga Makambo baada ya mshambuliaji huyo kuvunja mkataba wake uliosalia wa mwaka mmoja na sasa hatua hiyo ni kama inaongeza kasi ya Mkongomani huyo kukamilisha dili la kurejea Yanga.

Akizungumzia uwezekano wa Mayele kuunganika pamoja na Makambo ambaye Yanga wanamrudisha, Shungu alisema hiyo itakuwa ni pacha iliyokamilika endapo kocha wa Yanga atafanikiwa kuwaunganisha vizuri uwanjani.

Shungu ambaye aliwahi kuifundisha Yanga kwa mafanikio, alisema Makambo na Mayele wanajua kufunga, lakini kitu kibaya kwa timu pinzani ni kwamba wawili hao kucheza pamoja.

SOMA NA HII  YANGA KUWAFANYIA SAPRAIZI MASHABIKI ZAO LEO...CHICO, KOCHA WA SIMBA WATAJWA KUTAMBULISHWA...

“Unajua mabeki wengi ni wavivu, sasa Yanga wakiwa na Makambo anajua kukimbia na kufunga, Fiston naye yuko hivyohivyo na anapiga mashuti hata kwa mbali, hii itakuwa ni kitu kibaya kwa timu pinzani mabeki wao watapata shida sana.

“Itategemea lakini kama kocha wa Yanga (Nasreddine Nabi) atafanikiwa kuwaunganisha itakuwa ni safu bora ya ushindani ambayo Yanga watakuwa wakali kwa msimu ujao.

“Nawapongeza viongozi wa Yanga kama watafanikiwa kuwapata wachezaji hawa na kwa timu yao nilivyoiona sasa wanathibitisha kwamba wana watu ambao wanajua kuwatafutia wachezaji bora sio rahisi kuwa na wachezaji kama Tuisila (Kisinda), Mukoko ambao ni watu bora sana,” aliongeza kocha huyo.

Kama Yanga itamshusha Mayele na Makambo tafsiri yake ni kwamba itakuwa na Wakongomani watano kwenye kikosi cha kwanza msimu ujao. Wengine ni Djuma Shabaan, Tuisila na Mukoko.

Yanga imemaliza msimu huu ikiwa na pili katika msimamo nyuma ya watani zao, Simba.