Home Yanga SC MBALI NA BILIONI 8, HAYA HAPA MAMBO MAPYA 10 YATAKAYOIFANYA YANGA KUWA...

MBALI NA BILIONI 8, HAYA HAPA MAMBO MAPYA 10 YATAKAYOIFANYA YANGA KUWA YA KIMATAIFA


BAJETI iliyopitishwa na Yanga katika mkutano wake mkuu juzi huenda ikaifanya timu hiyo kuwa tishio katika mashindano ya ndani na hata yale ya kimataifa ikiwa mambo yataenda kama yalivyopangwa msimu ujao.

Katika mkutano huo mkuu uliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa DYCC, Dar es Salaam, Yanga ilitangaza na kupitisha bajeti ya Sh 8 bilioni kwa ajili ya msimu ujao wa 2021/2022.

Kudhihirisha imepania kuwa na kikosi tishio chenye wachezaji bora na wa daraja la juu, Yanga imetenga kitita kikubwa cha fedha takribani Sh 4.9 bilioni ambacho kitatumika kwa usajili na ulipaji wa mishahara kwa wachezaji, maofisa wa benchi la ufundi na maofisa wengine wa klabu.

Haiishii tu katika kusajili bali pia Yanga katika kuhakikisha inaongeza morali ya nyota hao itakaowasajili, imetenga kiasi cha zaidi ya Sh 854 milioni kwa ajili ya bonasi kwa wachezaji wake.

Lakini pia imetenga kitita cha zaidi ya Sh 201 milioni kwa ajili ya usafiri wa timu kwa safari za ndege za ndani na nje ukizingatia msimu ujao watashiriki mashindano ya klabu Afrika.

Wakati wakitangaza bajeti hiyo kibabe, Yanga imepiga bao lingine la kisigino baada ya wanachama wake kuridhia mabadiliko ya katiba na mfumo wa uendeshaji wa klabu hiyo.

MABADILIKO 10

Kati ya mengi yaliyofanywa katika katiba ya Yanga yanaonekana kubeba matumaini mapya ndani ya klabu hiyo kwa kutikisa zaidi hisia za wanachama, wapenzi na mashabiki wa klabu hiyo. Ni haya yafuatayo;

Kipengele cha kwanza kati ya hivyo 10 ni sifa za wagombea ambapo katiba mpya inalazimisha Rais wa Yanga kuwa na kiwango cha elimu kisichopungua ngazi ya shahada ya Chuo Kikuu huku wajumbe wa kamati ya utendaji wao wakitakiwa kuwa na angalau elimu ya kidato cha nne.

Lakini pia mbali ya kuwa mwanachama hai wa Yanga kwa kipindi kisichopungua miaka minne mfululizo, mgombea anapaswa kuwa na umri wa kuanzia miaka 25 na usiozidi miaka 75 lengo likiwa ni kuendana na mabadiliko yanayohitaji taaluma, ukomavu wa kifikra na uzoefu wa kibiashara na uendeshaji wa mpira wa kisasa.

Badiliko jingine walilopitisha juzi ni kupungua kwa idadi ya wajumbe wa mkutano mkuu ambapo tofauti na ilivyokuwa hapo awali kwamba mwanachama yeyote hai anaruhusiwa kushiriki mkutano mkuu, kwa sasa wawakilishi watano tu kutoka kila tawi ndio watapata fursa ya kuwawakilisha wengine katika mkutano mkuu.

Kuna ongezeko la gharama za kuwa mwanachama wa Yanga ni badiliko lingine ambalo wanachama wa klabu hiyo wanapaswa kulifahamu mapema kabla katiba mpya haijaanza kufanya kazi.

Tofauti na sasa ambapo gharama za kuwa mwanachama ni kiasi cha Sh 15,000 ambapo ada kwa mwaka ni Sh 12,000, Kadi Sh 2,000 na fomu Sh 1,000, gharama mpya ni Sh 36,000 ambapo ada ya mwanachama kwa mwaka ni Sh 24,000, kadi Sh 10,000 na fomu ni Sh 1,000.

Kuna mabadiliko katika ibara ya 28 ambayo ni kupungua kwa idadi ya wajumbe wa kamati ya utendaji kutoka 13 hadi tisa ambao watakuwa ni Rais wa klabu na makamu wake, wajumbe watano wa kuchaguliwa na wajumbe wawili wa kuteuliwa na Rais.

SOMA NA HII  FAINAL YA CAF YAGA MSIMU ULIPITA YAMFANYA KAMWE KUFUNGUKA HAYA KWA GAMONDI...

Ibara ya 33 inayofafanua kazi na majukumu ya Mwenyekiti na makamu wake, imefanyiwa pia mabadiliko ambapo sasa klabu itakuwa inaongozwa na Rais na sio mwenyekiti na makamu wake ambaye ameongezewa majukumu na sasa atakuwa mwenyekiti wa kamati ya fedha na mipango ya klabu lengo likiwa ni kuendana na mabadiliko ya mfumo na kuongeza udhibiti wa mamlaka za juu za klabu ya mipango na matumizi ya fedha.

Sekretarieti ya Yanga nayo imekumbwa na mabadiliko ambapo sasa itaitwa timu ya menejimenti huku ikipunguziwa idara hadi nne lengo likiwa ni kuleta dhana ya ubunifu na ufanisi.

Badiliko kubwa zaidi ni lile la ibara ya 56 ambapo Kampuni ya Umma ya Yanga itasomeka kama kampuni binafsi za Yanga ili kuifanya iweze kufungua kampuni zaidi ya moja.

Mgawanyo wa hisa katika kampuni hiyo utakuwa ni 51% zitamilikiwa na klabu na wawekezaji watamiliki 49%. Asilimia hizo 49 za upande wa wawekezaji zitagawanya kwa watu tofauti wasiozidi wanne na wasiopungua watatu ambapo kila mmoja atamiliki hisa zisizozidi 12.25%. Yanga kwenye mkutano wa juzi walipaaza sauti wakitaka Yusuf Manji (Mwenyekiti wa zamani), Rostam Aziz (mwanachama) na Ghalib Said ambaye ni miongoni mwa wadhamini wa sasa wachukue hisa hizo kurejesha heshima ya makombe Jangwani.

Itaundwa bodi ya kuendesha kampuni hiyo ambapo upande wa wanachama watawakilishwa na wajumbe watano ambao miongoni mwao watakuwa ni Mwenyekiti na Katibu Mkuu wa Klabu.

Badiliko la nane ni la ibara ya 55 ambapo tofauti na katiba ya sasa ambapo kamati ya utendaji inaweza kutoa mapendekezo ya kumfukuza mwanachama pasipo kushirikisha vyombo vingine, katiba mpya imeweka utaratibu ambao utaibana kamati ya utendaji katika kuchukua uamuzi kama huo ambapo saa utazingatia uamuzi na mapendekezo ya vyombo vya haki na vya kimahakama vilivyopo ndani ya klabu.

Jambo la tisa lililokumbwa na mabadiliko ni ibara ya tano, ambapo tofauti na awali ambayo ilikuwa inataja aina mbili tu za wanachama ambao ni wanachama kamili na wale wa heshima, sasa hivi katiba imeonyesha kuwatambua mashabiki ambao hawatohudhuria mkutano mkuu ambapo wanachama watakuwa na kadi za njano na mashabiki watakuwa na kadi za kijani.

Mabadiliko yaliyofanywa katika Ibara ya 62 inayohusu idadi ya wanachama ni jambo jingine ambalo bila shaka litagusa hisia za wanachama na mashabiki wengi wa klabu hiyo.

Tofauti na katiba ya sasa ambayo haijaweka ukomo wa idadi ya juu zaidi ya wanachama katika tawi moja huku ya chini ikiwa ni 100, katiba mpya imeweka ukomo kuwa namba ya wanachama katika tawi haipaswi kupungua watu 100 lakini haitakiwi kuzidiwatu 500.