Home Simba SC RAMANI YA SIMBA KUFUNGWA NA YANGA IMECHORWA NAMNA HII

RAMANI YA SIMBA KUFUNGWA NA YANGA IMECHORWA NAMNA HII


UNAKUMBUKA ile posho ya milioni 500 ambayo
 
uongozi wa Yanga uliwaahidi wachezaji na benchi la ufundi endapo wataifunga Simba katika mchezo wa Ligi Kuu na Yanga wakafanikiwa kuifunga?

Sasa unaambiwa matajiri wa Yanga wameweka kiasi hicho hicho ili waifunge tena Simba katika mchezo wafainali ya FA itayochezwa kesho Julai 25, mkoani Kigoma.

Hivyo ramani ya Simba kufungwa imechorwa na mabosi kupitia mkwanja mrefu uliowekwa mezani ikiwa wataweza kuwafunga watani zao hao wa jadi.

Yanga katika mchezo uliopita dhidi ya Simba walifanikiwa kuibuka na ushindi wa bao 1-0 katika mchezo wa mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Bara kwenye Uwanja wa Mkapa jijini Dar, huku mchezo wa safari hii katika fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam Sports ukitarajiwa kufanyika katika Uwanja wa Lake Tanganyika mkoani Kigoma.

Chanzo chetu cha ndani ya Yanga kimeliambia Championi Ijumaa kuwa uongozi wa Yanga umeweka ahadi kama waliyoiweka katika mchezo ule wa kwanza ambao Yanga ilifanikiwa kuibuka na ushindi wa bao 1-0 huku wakiamini pia kiasi hicho kitatosha kuwapa motisha wachezaji na kupata ari ya kupambana na kuibuka na ushindi dhidi ya wapinzani wao.

“Uongozi wa Yanga umetoa ahadi kama ile ya mwanzo ambayo ilisababisha Yanga iweze kuibuka na ushindi dhidi ya Simba, kama unakumbuka kiasi cha awali katika mchezo uliopita ilikuwa ni milioni 500 jambo ambalo na safari hii uongozi umeamua kuweka kiasi hichohicho.

“Sababu kubwa ya kufanya hivyo kwa viongozi wanaamini kuwa kiasi hicho kinatosha kuwapa wachezaji ari ya kupambana na kuipatia ushindi timu kama ambavyo ilivyotokea mara ya kwanza ambapo Yanga ilifanikiwa kuibuka na ushindi katika mchezo wa ligi,” kilisema chanzo hicho.

Alipotafutwa Dominick Albinus ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Yanga alisema kuwa ahadi na posho za wachezaji na benchi la ufundi la Yanga kuelekea katika mchezo wa Yanga zinabaki kuwa siri kutokana na mambo mbalimbali ambayo yamekuwa yakijitokeza baada ya ahadi hizo.

SOMA NA HII  SIMBA DHIDI YA AS VITA, MASHABIKI 10,000 RUKSA UWANJA WA MKAPA - VIDEO

“Kuhusu ahadi kuelekea mchezo wetu wa fainali dhidi ya Simba inabaki kuwa ni siri kati ya viongozi wa timu, benchi la ufundi na wachezaji kwani mara nyingi mara baada ya kutangaza ahadi mambo mbalimbali hujitokeza ambayo tumekuwa tukiyalaani sisi kama viongozi,” alisema kiongozi huyo.