Home news SIMBA WAIKIMBIA YANGA KIAINA MICHUANO YA KAGAME

SIMBA WAIKIMBIA YANGA KIAINA MICHUANO YA KAGAME

 


SIMBA haitoshiriki mashindano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame) yatakayofanyika Tanzania kuanzia Agosti Mosi hadi Agosti 15 mwaka huu kwa sabau ambazo hazijawekwa wazi.

Na badala yake, Tanzania Bara itawakilishwa na timu za Yanga na Azam FC ambazo tayari zimeshathibitisha kushiriki mashindano hayo makubwa kwa ngazi ya klabu yanayosimamiwa na Baraza la Vyama vyua Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (CECAFA).

Jumla ya klabu 10 zitashiriki mashindano hayo ambapo tisa ni kutoka nchi wanachama wa CECAFA na moja ni mualikwa ambayo ni Big Bullets ya Malawi.

Droo ya mashindano hayo imepangwa kuchezeshwa Jumanne, Julai 27 kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na CECAFA kupitia kwa mtendaji mkuu wake, Auka Gecheo.

Timu hizo 10 ambazo zitashiriki mashindano hayo ni Yanga na Azam za Tanzania, Altabara FC (Sudan Kusini), Le Messager Ngozi (Burundi), APR (Rwanda), Express na KCCA (Uganda), Tusker (Kenya), KMKM (Zanzibar) na Big Bullets (Malawi).

Mtendaji huyo mkuu wa CECAFA alisema wanaamini mashindano hayo yatakuwa kipimo kizuri kwa timu za ukanda wa Afrika Mashariki na Kati katika kujiandaa na mashindano ya klabu Afrika.

“Mashindano haya yatazisaidia timu za ukanda wetu kujiandaa na mashindano ya klabu Afrika yatakayoanza Septemba. Tutakuwa pia na timu mgeni kutoka Malawi kunogesha mashindano,” alisema Gecheo

KCCA ndio mabingwa watetezi wa mashindano hayo ambapo walitwaa taji hilo mwaka 2019 yalipofanyikia Rwanda ingawa mwaka jana hayakufanyika kutokana na changamoto ya ugonjwa wa Covid-19

SOMA NA HII  'GOLI LA MKONO' LAMTOKEA PUANI FEI TOTO...NABI ASHINDWA KUJIZUA...AFANYA MAAMUZI HAYA..