NYOTA wa Simba, Joash Onyango amesema kuwa wale ambao walikuwa wanambeza msimu huu uliomeguka wa 2020/21 kwamba ni mzee wameona kazi aliyofanya na mwisho wa siku wameweza kukaa kimya.
Onyango ambaye ni ingizo jipya ndani ya Simba aliibuka hapo akitokea Klabu ya Gor Mahia ya Kenya.
Wakati anatua Simba mashabiki wengi wa timu pinzani pamoja na wale wa timu yake baadhi walikuwa wakieleza kwamba umri umekwenda na ni mzee hivyo hataweza kufanya vizuri.
Kwa msimu huu ni miongoni mwa mabeki bora ndani ya ligi kwa sababu timu ya Simba imefungwa mabao machache ambayo ni 14 baada ya kucheza mechi 34.
Onyango amesema:”Nilikuwa ninawaskia wakiniita mzee hilo ni sawa kwa kuwa wao walikuwa wameamua na waliona hivyo haina tatizo.
“Kwa ajili ya kile ambacho nimefanya wamekaa kimya hawajaniita mzee tena hivyo msimu ujao tena Mungu akipenda nikiwa hai basi nitapambana zaidi,” amesema.
Kwa msimu wa 2020/21 alikuwa ni chaguo la kwanza la Kocha Mkuu, Didier Gomes na hata zama zile za Sven Vandenbroeck alikuwa chaguo la kwanza.
Amenyanyua makwapa mara nne kwa kuanza na Ngao ya Jamii, Simba Super Cup, Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho.