Home Makala OSCAR OSCAR : TATIZO SIO CHAMA NA LUIS KUONDOKA SIMBA..TATIZO NI….

OSCAR OSCAR : TATIZO SIO CHAMA NA LUIS KUONDOKA SIMBA..TATIZO NI….


Hakuna timu bora duniani iliyowahi kufanikiwa kwa kuwauza wachezaji wake bora. Haipo. Timu zote bora zimekuwa na utamaduni wa kuwazuia wachezaji wake bora kuondoka.

Zaidi ya miaka 20, FC Barcelona walikuwa na Lionel Messi. Zaidi ya miaka tisa, Real Madrid haikuruhusu Cristiano Ronaldo aondoke.

Ndiyo msingi wa timu zote bora. Ndiyo msingi wa kuwa timu kubwa. Pale ndani ya Wekundu wa Msimbazi Simba ni suala la muda tu, Clatous Chota Chama na Luis Miquessone wako njiani kuondoka ndani ya klabu hiyo.

Biashara ni kuuza na kununua wachezaji duniani kote lakini mashabiki wa Simba wako tayari katika hili? Nitumie maoni yako kupitia namba yangu ya simu hapo juu.

Chama amekuwa mchezaji muhimu sana ndani ya Simba. Ndiyo Ronaldinho Gaucho wao. Ndiyo Zinedine Zidane wa Simba kwa Kizazi hiki. Luis Miquessone amekuwa tegemezi sana ndani ya Simba.

Ndiyo Kyllian Mbappe wa Simba.

Ndiyo Sadio Mane wa Simba wa Kizazi hiki. Ni kweli soka ni biashara lakini, wana Simba mko tayari kuondokewa na mastaa wawili kwa wakati mmoja? Usisite kunipa maoni yako kupitia namba yangu ya simu hapo juu.

Bado Simba hawajatangaza rasmi lakini habari ndiyo hiyo. Ni sula la muda tu. Muda wowote taarifa rasmi itatoka juu ya kuuzwa kwa Luis Miquessone na Clatous Chota Chama.

Tuko tayari kwa biashara ya soka? Simba waliwahi kuwa na Mbwana Samatta kama shujaa wao, japo kwa muda mfupi lakini aliuzwa na mashabiki wakatulia.

Simba iliwahi kuwa na shujaa wao Emmanuel Okwi, naye aliuzwa na mashabiki wakatulia. Zama zimebadilika. Simba imebadilika na biashara ya wachezaji imebadilika pia.

Kama unaweza kumnunua mchezaji kwa Dola 100,000, ikitokea timu inamtaka mchezaji huyo baada ya msimu miwili kwa Dola 500,000, ukiziacha wewe utakuwa na tatizo.

Ukiziacha wewe utakuwa hujui biashara ya soka. Hapa kuna shida moja tu kubwa, ni kupata mbadala wa wachezaji hao.

Hakuna kitu kigumu kwenye soka kama kusajili. Usajili una kanuni zake lakini hakuna mwenye uhakika wa mchezaji mwingine kuja kufanya vizuri.

Simba wanaweza kumleta hata Kyllian Mbappe kama mbadala wa Miquessone na akachemsha! Simba wanaweza kumleta hata Harry Kane na akashindwa kufanya vziuri.

Ndiyo usajili wa soka ulivyo. Ndiyo changamoto za soka. Biashara ya soka inawalazimu Simba kuwauza wachezaji wake tegemeo kipindi wanahitaji kujijenga zaidi.

Kwa hiki kinachoenda kutokea Simba, ni mchezo wa kamari! Hakuna anayejua kama Simba watakula katika hili au wataliwa! Tatizo sio kuwauza Chama na Miquessone, shida ipo kwenye kupata mbadala wao.

Siku zote tumekuwa tukisema soka ni biashara kubwa, lakini tuko tayari kwa biashara hiyo? Unaweza kunipa maoni yako kupitia namba yangu ya simu hapo juu.

SOMA NA HII  MCHEZAJI MAMELODI APATWA NA KICHAA...ANAISHI CHINI YA DARAJA...INASIKITISHA SANA

Kumpoteza Chama msimu ujao na Miquessone ni mtihani mkubwa kwa Simba.

Lakini Simba wamekuwa na watu nguli sana linapokuja suala zima la usajili. Sina shaka hata kidogo na kaka yangu Crescentius Magori na Mzee wangu Zacharia Hans Poppe.

Hawa ni baadhi ya watu wanaofanikisha usajili wa Simba.

Baada ya kufika hatua ya Robo Fainali ya Afrika mara mbili katika kipindi cha miaka minne ya hivi karibuni, Simba walihitaji zaidi nguvu ya kwenda nusu fainali lakini sio Kwa kuwauza Chama na Miquessone.

Hawa ni wachezaji bora ndani ya Kikosi ambao walipaswa kuongezewa zaidi nguvu. Walipaswa kuongezewa zaidi makamanda wapya ili kufikia lengo lakini, ndiyo biashara ya soka ilivyo. Tabia ya samaki wakubwa kumeza wadogo iko pale pale kwenye soka.

Ni vigumu sana kwa timu zetu na wachezaji wetu kukataa ofa ya timu kama Al Ahly. Hawa ndiyo Real Madrid wa Afrika. Ni vigumu sana kwa klabu zetu kukataa ofa kutoka Mataifa ya Afrika ya Kaskazini. Misiri, Morocco, Tunisia na Algeria wamepiga hatau kubwa sana kisoka. Kuanzia miundombinu mpaka mishahara. Maana halisi ya Mpira Pesa iko kule.

Maana halisi ya watu wa soka iko kule. Sina tatizo na Simba kuwauza wachezaji wake muhimu, nina mashaka na mbadala wa wachezaji wataosajiliwa. Ndiyo biashara ya soka. Ndiyo Utamaduni wa soka, wachezaji watauzwa tu.

Simba imekuwa bingwa mara nne mfululizo, haikuwa kwa bahati mbaya. Simba wamekuwa na timu bora. Simba imekuwa na wachezaji bora.

Lakini kwa kumkosa Luis na Chama, Simba watatetereka. Wanapawa kuchanga vyema sana karata zao kwenye usajili. Natazama washindani wa karibu wa Simba hapa nyumbani, Yanga na Azam , naona wamepania kuelekea msimu mpya.

Azam FC wamefanya usajili wa moto sana. Yanga ndiyo usiseme. Ni kama wana hasira hivi! Kila kukicha wameshusha watu.

Pamoja na Simba kuwa bora karibu kwenye kila kitu dhidi ya wapinzani wao, lakini kitendo cha wachezaji wao wengi kucheza pamoja kwa muda kuliongeza tofauti yao na wapinzani wao. Kwa kuondoka kwa Miquessone na Chama ni kama Simba nao watakuwa wanajenga timu.

Kuna kazi kubwa sana inapaswa kufanywa na hasa kwenye kamati ya usajili. Simba watajikuta nao wanakuwa na upya kwenye kikosi chao. Sawa na Yanga. Sawa na Azam. Kifupi, kuondoka Kwa Miquessone na Chama Kunaacha wazi mbio za ubingwa wa ligi Kuu Bara kuelekea msimu ujao.

Kuondoka Kwa Miquessone na Chama, kunaacha pia wasiwasi kama Simba itakuwa tishio tena kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika. Ni Taarifa chungu lakini ndiyo biashara ya soka.

IMEANDIKWA NA OSCAR OSCAR