Home Makala HUU HAPA UJUMBE WA MWISHO WA MWL KASHASHA KWA SOKA LA TZ..AZITAJA...

HUU HAPA UJUMBE WA MWISHO WA MWL KASHASHA KWA SOKA LA TZ..AZITAJA SIMBA NA YANGA


MSIMU wa 2020/2021 umekamilika tukiwa tumeshuhudia mengi yaliyojiri katika viwanja vya soka ambapo wapo waliofanya vizuri na ambao hawakuweza kutimiza malengo.

Katika kipindi hiki baada ya msimu kumalizika, timu zipo kwenye maandalizi kwa ajili ya msimu ujao hivyo zinajipanga kujiimarisha kwa kubadili baadhi ya wachezaji na watu katika management.

Yanga ni timu kubwa na imeonekana kustruggle katika msimu uliomalizika hivyo katika kipindi hiki nayo imekuwa inajiimarisha kwa kupunguza baadhi ya wachezaji na kusajili wengine.

Kwenye kujiimarisha huko, Yanga imeachana na wachezaji kadhaa na miongoni mwao ni kiungo Haruna Niyonzima na beki ambaye pia alikuwa nahodha wao, Lamine Moro.

Tukianza na Haruna Niyonzima, huyu alikuwa mchezaji kipenzi kwa mashabiki wa Yanga lakini pia wadau wa soka nchini kutokana na aina yake ya uchezaji.

Kuna mambo mawili ambayo yamechangia Niyonzima kugeuka kipenzi kwa Wanayanga na mashabiki wa soka hapa Tanzania kwa kipindi chote alichocheza cha takribani miaka nane.

Kwanza ni mchezaji ambaye anacheza kwa kutegemea kipaji chake. Alikuwa na uwezo wa kuamua kwa haraka apeleke wapi mpira na awaadae vipi wapinzani pindi timu yake ilipokuwa ikishambulia ama kumiliki mpira.

Wote tunafahamu kuwa alikuwa nahodha wa timu ya taifa ya Rwanda hivyo alikuwa na sifa ya uongozi ambayo alijitahidi kuitumia katika kusaidia wenzake.

Lakini jambo lingine ni kwamba Haruna alikuwa anacheza mpira huku akiwa anautaka. Alikuwa anafanya kitu anachokipenda akiwa ndani ya uwanja.

Ni mchezaji ambaye alikuwa na uwezo wa kuichezesha timu. Anaweza kugeuza uelekeo wa mpira na alikuwa anaamua timu icheze vipi.

Kuna nyakati, Yanga ilikuwa inacheza kwa kumzunguka yeye na ndio alikuwa kama dereva wa kuamua aina ya soka la kucheza inapokuwa uwanjani. Akitaka ikimbie ilikuwa inakimbia na akitaka timu icheze taratibu, ilikuwa inafanya hivyo.

Kwa hiyo niseme tu wazi kuwa tutakosa taste ya Niyonzima mara baada ya kuondoka kwake kwani ni mara chache sana unaweza kuwapata wachezaji wa aina yake.

Ingawa anaondoka, bado ni mchezaji mzuri na naamini anaweza kupata timu nyingine na akaonyesha kiwango bora na kuwa msaada.

SOMA NA HII  HUU HAPA NDIO USAJILI UTAKAOSUMBUA ZAIDI LIGI KUU IKIANZA...BIGIRIMANA, PHIRI, AZIZ KI NA OKRAH WOTE NDANI....

Mwisho wa siku tumtakie kila la kheri huko aendako na tumshukuru kwa mchango mkubwa alioutoa kwa soka letu katika kipindi chote alichocheza hapa nchini katika timu za Yanga na Simba

Ukiondoa Haruna Niyonzima, Yanga pia imetangaza kuachana na nahodha na beki wake wa kati, Lamine Moro ambaye ilimsajili mwaka 2019 akitokea Buildcon ya Zambia kama mchezaji huru.

Lamine Moro kabla ya kujiunga Yanga, alianza kufanya majaribio Simba ambayo haikuridhishwa na kiwango chake na kuamua kutomsajili kabla ya upande wa pili kuamua kumsajili.

Baadaye alionekana ni mchezaji mzuri na mwenye ufanisi mkubwa kiwanjani akiwa na sifa nyingi za beki wa kati ambazo ni footwork, speed, uwezo wa kucheza mipira ya juu na ya chini lakini pia ni mchezaji ambaye ana uwezo wa kufunga pale aliposogea jirani na lango la adui.

Hata hivyo upande mmoja wa shilingi kulionekana kuna shida kidogo akidaiwa kuwa na tatizo la kinidhamu lakini hili linafikirisha kidogo maana hapa nchini wakati mwingine mchezaji akiwa na madai fulani anaonekana ana matatizo.

Lamine alikuwa ni mlinzi kiongozi nje na ndani ya uwanja na kwa aina ya uchezaji wake, nadhani bado alikuwa anahitajika kikosini.

Commitment yake ni ya hali ya juu mno. Kiutendaji uwanjani alikuwa na msaada mkubwa na naona nafasi ya kucheza bado alikuwa nayo lakini kwa vile uongozi umeshaamua, inabidi tuheshimu uamuzi wao.

Alikuwa na nafasi ya kuendelea kucheza na sina shaka atapata timu mahali pengine.

Japo amecheza kwa muda wa miaka miwili, Lamine Moro kwa nafasi yake ametoa mchango mkubwa kwa soka letu na naye inapaswa tumpongeze na kumtakia kheri katika maisha yake mapya nje ya Yanga.

Kiujumla, wachezaji wetu wazawa hasa wale wenye umri mdogo, wanapaswa kujifunza na kuyachukua yale mazuri ya Lamine Moro na Haruna Niyonzima kwa faida yao siku za usoni.

ILIANDIKWA NA ALEX KASHASHA