YANGA bado haijaanza kivile mazoezi ya uwanjani, lakini wamepokea maombi ya timu mbili zikitaka kutesti nao mitambo.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Yanga, Hersi Said alisema ndani ya siku mbili tu tangu wafike hapa wamepokea maombi ya timu mbili zikiomba kujipima nao kabla ya muda wa kufunga kambi.
Hersi alisema timu hizo mbili zote ni za hapa Morocco, lakini hata hivyo ratiba yao bado haijaamua kama ni lini wataamua kucheza ama kutocheza mechi hizo.
“Suala la mechi za kirafiki niseme tu mpaka sasa tuna maombi ya klabu mbili za hapa, zimeomba tucheze nao mechi za kirafiki, hizo ni zile zenye uhakika na kwamba sisi tu tuamue,” alisema Hersi bila kutaja majina ingawa Raja Casablanca ni mojawapo.
Hersi aliongeza hata hivyo wao kama viongozi hawana uamuzi wowote katika hilo na badala yake uamuzi wa mwisho ameachiwa kocha mkuu Nesreddine Nabi ambaye ndiye ataamua kulingana na ratiba yake.
“Tumempelekea maombi hayo kocha ataangalia sasa anahitaji kipi, sisi hatuna cha kulazimisha ataangalia kulingana na muda tutakaokuwa hapa ni lini anaweza kuhitaji na bado hajatuambia chochote kuhusu kuhitaji mechi hizo,” alisema.
Yanga imemaliza siku ya pili ya mazoezi ya uwanjani wakishafanya vipindi vinne ya mazoezi kwa asubuhi na jioni wakiwa jijini Marrakech nchini Morocco walikoweka kambi ya maandalizi ya msimu mpya wa Ligi Kuu Bara.