KOCHA wa Yanga amewaangalia vijana wake akawaambia mashabiki kwamba; “sasa hii ndiyo Yanga niliyoitaka.”
Kocha Nesreddine Nabi alisema usajili ambao umefanywa na matajiri wao wa GSM umemfurahisha na sasa amepata timu sahihi itakayokuwa na sura sahihi ya kupigania mataji.
Nabi ambaye ana uraia wa Ubelgiji na Tunisia, alisema katika mazoezi ya juzi na jana walipocheza mpira kwa mara ya kwanza tangu waanze kambi yao amegundua kwamba Bilionea wa GSM Ghalib Mohamed amekamilisha kazi yake ya kuijenga Yanga imara na sasa kazi inabaki kwake.
“Nimewaangalia wachezaji niliwaambia subirini kwanza nione kwa umakini ubora wa wachezaji ambao wamesajiliwa na sasa niseme msimu ujao tutakuwa na timu imara ambayo itakwenda kupigania heshima ya mataji ya Yanga.
“Niliongea na Ghalib kabla ya msimu kumalizika aliniahidi atasajili timu imara na sasa nimeona kweli amekamilisha ahadi yake kwangu na sasa ni kazi yangu na wasaidizi wangu pamoja na wachezaji sasa kuthibitisha ubora wao, hili ni kundi la wachezaji waliokomaa,” alisema
Hata hivyo Nabi amelia na muda akisema hata kama wamepata wachezaji bora haitakuwa haraka kwasasa kuanza kuona matunda kutokana na muda mfupi wa maandalizi kabla ya kuanza mashindano.
Nabi alisema ratiba ya wachezaji wake kurudi timu za taifa lakini pia muda mfupi kabla ya kuanza mechi za Ligi ya Mabingwa zitaifanya Yanga anayoitaka kuchelewa kuiva kimaandalizi ambapo amewataka mashabiki kutulia na kumpa siku 90 tu waanze kuona mafanikio makubwa.
“Tuna kundi la wachezaji wapya ambao ni wengi lakini ukiangalia ligi ilichelewa kumalizika na sasa muda wa maandalizi umekuwa mchache, muda si mrefu kundi kubwa la wachezaji litatawanyika tena na kurudi katika mataifa yao,” alisema Nabi.
“Wakirudi tutakuwa na siku chache tena kabla ya kuanza mechi za Ligi ya Mabingwa tukianza nyumbani kisha ugenini utaona jinsi mambo yanavyobana lakini niwaambie mashabiki watulie waniachie kazi wasiongeze presha kwa wachezaji, ndani ya siku 90 wataona kitu kikubwa hapa,” aliongeza kocha huyo ambaye timu yake inaanza nyumbani kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Rivers United ya Nigeria, Septemba 11.