KLABU ya Yanga inatarajia kucheza mchezo wa kirafiki na timu ya Zanaco FC ya Zambia katika siku ya Mwananchi ikiwa ni kuelekea maandalizi ya msimu mpya.
Mchezo huo unatarajiwa kucheza Agosti 29 baada ya timu hiyo kuzindua siku ya Mwananchi Agosti 22 visiwani Zanzibar ambapo lengo kubwa ni kushiriki shughuli mbalimbali za kijamii.
Ofisa habari na mawasiliano wa Yanga Hassan Bumbuli amesema kuwa wanatarajia kucheza na Zanaco kwa sababu ni timu imara itakayoleta ushindani katika kikosi hicho.
“Tunatarajia kucheza na Zanaco FC katika mchezo wa kwetu wa kirafiki na watawasili nchini Agosti 27, lengo kubwa ni kutoa fursa kwa mashabiki wetu kuona kikosi chetu na maandalizi kwa ujumla,” amesema.
Tamasha hilo litahudhuriwa na msanii wa muziki aina ya dansi, Koffi Olomide ambaye atakuwa ni mmoja wapo wa wasanii watakaotumbuiza katika siku ya Mwananchi itakayofanyika Agosti 29 katika Uwanja wa Mkapa Jijini Dar es Salaam.
Awali Mwenyekiti wa kamati ya habari na hamasa na mjumbe wa kamati ya utendaji Yanga, Suma Mwaitenda alikaririwa na Mwanaspoti online akisema kuwa tamasha hilo licha ya kuwa na wasanii wengi ila wataongozwa na Koffi Olomide.
“Tutakuwa na Namba ambayo itakuwa inaweka statasi kwenye simu na kuonyesha kila ratiba ya tukio itakavyokuwa, hii ni timu ya wananchi na namba hii itawasaidia wanachama kupata ratiba,” alisema Mwaitenda.
Viingilio katika siku ya Wananchi wa chini itakuwa ni Sh3000 na kiwango cha juu ni Sh200, 000 ambao watakuwa na uangalizi mwingine.