Kipa wa Simba, Beno Kakolanya amewaomba mashabiki kuendelea kuisapoti timu hiyo ili msimu ujao wazidi kufanya vizuri na kubeba mataji kama walivyofanya msimu uliopita.
Kakolanya ambaye alikuwa jijini hapa kutokana na matatizo yaliyomkuta ya kufiwa na mama yake mzazi, anatarajia kurudi Dar es Salaam leo Jumatatu kuungana na wenzake kikosini tayari kwa maandalizi ya msimu ujao unaotarajia kuanza mwishoni mwa mwezi Septemba.
Akizungumza jana Jumapili Agosti 29 wakati wa uzinduzi wa tawi la Simba Unyamwanga wilayani Rungwe mkoani hapa, Kakolanya amesema wachezaji wanatambua sapoti kubwa kutoka mashabiki na kuwaomba kuendelea kuwapa nguvu.
Amesema matarajio yao ni kufanya vizuri msimu ujao na kubeba makombe kama walivyofanya msimu uliopita na kuwaomba kuendeleza umoja ndani ya timu.
“Kwa niaba ya wachezaji wote wa Simba niwaombe sapoti yenu kuendelea wakati tukijiandaa na msimu ujao kuhakikisha tunabeba tena makombe yote kama ilivyokuwa msimu uliopita” amesema Kakolanya.
Kipa huyo namba mbili kwa Wekundu, ametumia pia muda huo kuwashukuru mashabiki wa timu hiyo mkoani hapa kwa sapoti waliyompa wakati wa kipindi chote cha msiba wa mzazi wake akisema kuwa hawezi kuwalipa chochote.
“Kiujumla niwashukuru sana mashabiki na wadau wengine ambao walikuwa namimi kwa muda wote, sina cha kuwalipa Mungu awabariki” amesema Kipa huyo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Simba mkoani hapa, Abel Edson amesema matumaini yao kwa Kipa huyo msimu ujao atakuwa bora kwani baraka alizopata kwa mashabiki zitampa maendeleo mazuri.
“Leo Beno una baraka kubwa sana na tunakuombea ukapate mafanikio makubwa ndani ya timu na wewe binafsi, ulichokifanya msimu uliopita kiwe zaidi msimu ujao” amesema Edson.