KOCHA Mkuu wa Simba, Didier Gomes amemuwekea ngumu kiungo mkabaji wa timu hiyo, Jonas Mkude kwa kumtaka abadilike juu ya matukio yake ya utovu wa nidhamu kwa kumpa onyo kali pamoja na kumuweka chini ya uangalizi wake.
Mkude ambaye mwishoni mwa msimu uliopita, aliingia katika mzozo na benchi la ufundi la timu hiyo pamoja na wachezaji wenzake kutokana na kufululiza kwa matukio yake ya utovu wa nidhamu kiasi cha uongozi wa timu hiyo kumsimamisha kwa muda hadi kupelekwa kwenye Kamati ya Nidhamu ya Simba chini ya Kamanda mstaafu wa Dar es Salaam, Seleman Kova.
Taarifa za uhakika kutoka Simba, zinaeleza kuwa Gomes ameamua kumuweka chini kiungo huyo na kumpa masharti yake ikiwa atahitaji kuendelea kucheza Simba.
Mtoa taarifa huyo alienda mbali zaidi kwa kusema Gomes alitoa masharti hayo kwa kuwa hataki kuwagawa wachezaji wake kupitia matatizo ya utovu wa nidhamu kwani mipango yake ni kishughulikia kwenye levo moja.
“Ni kweli mwalimu Gomes, alikaa kikao na Mkude hii ni kutokana na masuala yake la utovu wa nidhamu, amempa masharti kwa kuwa mwalimu hataki kuona anaigawa timu upande wa wachezaji ambao mwenyewe anataka wawe kwenye daraja moja ili kuweza kupambania timu.
“Mwalimu amemuambia hataki kusikia jambo lolote la utovu wa nidhamu kutoka kwake kama alivyofanya msimu uliopita, amemwambia anataka kumuona wa kwanza katika kila jambo ambalo timu hiyo itakuwa inafanya kwa wakati huo,” alisema mtoa taarifa