WAKATI Yanga ikipoteza mechi yake ya kwanza ya kirafiki dhidi ya Zanaco jana kwa kufungwa bao 2-1, wapinzani wao kwenye kwenye michuano ya kimataifa, Rivers United ya Nigeria jana imeshinda 1-0 dhidi ya Akwa United.
Yanga na Rivers zitakutana Septemba 12 kwenye mchezo wa awali wa Ligi ya Mabingwa Afrika kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam.
Katika mechi ya Yanga bao la Yanga lilifungwa na mchezaji mshambuliaji wake mpya Heritier Makambo kwenye kipindi cha kwanza kabla ya kipindi cha pili Zanaco kusawazisha na kuongeza kupitia kwa Ackim Mumba na Kelvin Kapumbu.
Bao la wapinzani wa Yanga kwenye Ligi ya Mabingwa lilifungwa na Fortune Omoniwari dakika ya tisa ya mchezo huo baada ya kupokea pasi kutoka kwa winga Ishaq Kayode.
Na dakika ya 66 kipa wa Rivers, Theophilus Afelokai alionesha umahili wake wa kudaka kwa kuokoa mkwaju wa penati wa Akwa United na kuifanya timu yake ishinde 1-0 kwenye mechi hiyo iliyopigwa katika Dimba la Adokiye Amiesimaka.