Home Yanga SC BREAKING…KIGOGO YANGA AMBWAGA MANYANGA… AMTAJA MANARA..AFUNGUKA HAYA..

BREAKING…KIGOGO YANGA AMBWAGA MANYANGA… AMTAJA MANARA..AFUNGUKA HAYA..

SAA chache tu baada ya aliyekuwa Msemaji wa Simba, Haji Manara kujiunga na Yanga, Kigogo wa klabu hiyo na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya klabu hiyo, Athuman Kihamia ametangaza kujiuzulu na ameweka bayana kilichomfanya achukue uamuzi huo huku akimzungumzia Manara.
Kihamia ambaye ni Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha alisema kuwa uamuzi wake wa kuachia ngazi ndani ya Yanga unatokana na kubanwa na majukumu ya kiserikali.
Kigogo huyo ambaye ni mmoja kati ya watu wenye ushawishi na wakongwe ndani ya Yanga alisema hatua ya kuondoka kwake ndani ya Yanga ilikuwa ni kiu yake ya muda mrefu na mara kadhaa aliwahi kupeleka maombi kwa Mwenyekiti wa klabu hiyo, Dk Mshindo Msolla.
“Ni kweli nimeamua kukaa kando kidogo, unajua Yanga ni klabu yangu ninayoipenda na kwa sasa majukumu yangu yamekuwa mengi sana, huku Arusha kuna kazi za kiserikali zinaninyima muda wa kujua mengi yanayoendelea klabuni, sasa huwa sitaki kufanya kazi ya kulipua,” alisema Kihamia.
“Wakati nakubali majukumu haya muda mwingi nilikuwa sana Dar es Salaam ambako ndio makao makuu ya klabu lakini pia vikao vingi huwa tunavifanyia pale, ila sasa niko huku Arusha nakosa muda wa kutosha kufuatilia yale ambayo yalikuwa yanatakiwa niyafanye, kuendelea kung’ang’ania nafasi ni kutowatendea haki wanachama wenzangu.”
Aidha, Kihamia amefafanua uamuzi wake wa kuondoka hauna uhusiano na kitendo cha Manara kutambulishwa Yanga ambapo utambulisho huo ameusikia tu kupitia vyombo vya habari mara baada ya kurejea nyumbani katika majukumu yake.
Alisema hawezi kuumizwa wala kuchukia hatua hiyo sababu Yanga ina uongozi na inawezekana zipo sababu za msingi zilizozaa uamuzi huo kwa faida ya klabu.
“Nimekwambia kwamba majukumu yangu ni mengi sana ni vile mimi ni mtumishi wa serikali tuna miiko yetu ya kuweka wazi mambo ya serikali lakini hivi ninavyokwambia nimeona hii taarifa muda si mrefu kupitia mitandao ya habari tu nikiwa nimerejea hapa nyumbani,” alisema Kihamia na kuongeza;
“Kusema kweli sikuwa najua hicho kitu lakini inawezekana mimi niko huku Arusha sasa wenzangu walioko kule (Dar es Salaam) wanaweza kuwa walishirikishwa na siwezi kutangulia kupinga kwa kuwa sijajua waliofanya uamuzi huu waliangalia kipi chenye faida kwa klabu yetu.
“Inawezekana zipo faida Yanga ina uongozi wameona Manara anaweza kuja kusaidia klabu sasa wangetafutwa wenzangu au ikiwezekana uongozi wa juu na wajumbe wenzangu wengine wanaweza kulifafanua hili kwa kina,” alisema.

SOMA NA HII  YANGA: HATUNA HOFU NA SIMBA