Home Cecafa Cup KAGAME INATUUMBUA KWENYE UWEKEZAJI WA VIJANA, RATIBA YETU

KAGAME INATUUMBUA KWENYE UWEKEZAJI WA VIJANA, RATIBA YETU


TIMU nne tayari zimetinga hatua ya nusu fainali katika Kombe la Kagame 2021 ambalo linafanyika Tanzania.Mwanzo wa mashindano ni timu nane zilianza kasi ya kusaka nafasi ya kutinga katika hatua ya fainali.

Kwa Tanzania ilikuwa ni timu tatu ambazo zilikuwa zinapeperusha bendera kwenye haya mashindano ilikuwa ni Azam FC, KMKM na Yanga.

Hapo ndipo unaona kwamba kuna timu ambazo zililialikwa na kusepa kimyakimya kwa kile ambacho kilielezwa kuwa ni ratiba kuwabana, hiyo ni sawa kwa kuwa ni maamuzi yao.

Tumeona kwa timu ambazo zimeshiriki asilimia kubwa walikuwa wanatumia vijana katika kusaka ushindi. Jambo ambalo linatoa picha kwamba hata timu ambazo ziliweka sababu bado zilikuwa na nafasi ya kushiriki.

Upande wa Simba ambao wanasema kwamba wana kikosi kipana waliweza kujiweka kando lakini nina amini kwamba licha ya ratiba kuwa ngumu kwao bado walikuwa wananafasi ya kuwaruhusu vijana wao waweze kucheza katika mashindano haya.

Kama ambavyo Yanga walifanya kwa kuwaruhusu vijana wao waweze kucheza na mwisho wa siku walipata kile ambacho walistahili kwa kuwa mchezo wa mpira ni mchezo wa wazi.

Nyota wao kutoka timu ya vijana pamoja na wale kutoka timu ya wakubwa ambao walikuwa hawapati nafasi waliweza kuonyesha uwezo wao.

Mbivu na mbichi ziliweza kuonekana kwa kuwa wale ambao walikuwa wakihitaji kumuona Wazir Junior akifanya yake wamemuona ndani ya mechi zake tatu kasepa na bao lake moja.

Ukweli ni kwamba licha ya kwamba muda ulikuwa mdogo bado kulikuwa na faida kwa wachezaji wengine kupewa nafasi kushiriki hasa kwa wale ambao walikuwa hawapati nafasi.

Kwa mfano kuna kikosi cha vijana Simba ambacho hakikuwa na mashindano basi busara ingetumika kwa ajili ya kuongeza nguvu kwa wawakilishi wa Tanzania kwenye mashindano haya makubwa.

Ushiriki wa vijana ungezidi kuongeza wigo kwa vijana ambao hawaonekani kupata nafasi ya vipaji vyao kuzidi kuwa sokoni pia wale wachezaji wengine ambao walikuwa hawapati nafasi kikosi cha kwanza ingekuwa ni muda wao kuweza kuonekana .

SOMA NA HII  TANZANIA U18 YATAMBA UBINGWA CECAFA

Yupo beki Gadiel Michael rekodi zinaonyesha kuwa ni mechi tatu alicheza kati ya 34 huku kipa namba tatu Ally Salim akiwa hajacheza mchezo hata mmoja ilikuwa ni fursa kwao kuweza kuonyesha nguvu ya vijana wao kwenye mashindano haya.

Kwa matokeo ambayo Azam FC walikuwa wakiyapata kupitia vijana wao inatupa picha kwamba kuna nguvu kubwa kwa timu hiyo katika hilo wanastahili pongezi sawa na KMKM.

Ukija kwa Yanga mambo inaonekana bado kwani walikuwa wanapambana muda wote kusaka matokeo licha ya kwamba walikuwa na mashabiki wao uwanjani.

Matokeo yanatuumbua Watanzania katika uwekezaji wa vijana ambao ni taifa la kesho kwenye ulimwengu wa mpira. Jambo la msingi kuwe na nguvu kubwa kwa timu zote kuwanoa vijana.

Mashindano kama haya yanapotokea ni fursa ya kuwapa vijana muda wa kucheza. Pia inaonyesha kwamba namna upangaji wa ratiba na kutimia kwake unavyowambana wachezaji kunafanya washindwe kupata muda wa kupumzika.

Zipo timu ambazo zimeshiriki Kagame zikiwa zinafanya maandalizi kwa ajili ya msimu ujao lakini kwa Tanzania ni muda ambao wachezaji wanapaswa kupumzika.

Kwa haya ambayo yanatokea basi ni muhimu kuwe na mabadiliko kwa wakati ujao kuanzia kweye upangaji wa ratiba pamoja na uwekezaji kwa vijana.