Home Makala MAANDALIZI YA MSIMU UJAO NI MUHIMU ILI KULETA USHINDANI

MAANDALIZI YA MSIMU UJAO NI MUHIMU ILI KULETA USHINDANI


 KUKAMILIKA kwa msimu wa 2020/21 kunaamanisha kwamba ni mwanzo wa msimu mpya wa 2021/22 ambao unatarajiwa kuanza hivi karibuni.

Ule mpango mrefu wa Shirikisho la Soka Tanzania, (TFF) katika kupunguza idadi ya timu ambapo kwa msimu huu zilikuwa 18  ulikuwa unaendelea na tayari umekamilika.

Kwa msimu ujao zitakuwa timu 16 baada ya nne kushuka jumlajumla msimu huu.

Kushuka kwa timu nne ni muhumu kwa wale wachezaji ambao wameshuka na timu kuweza kuangalia namna ambayo wanaweza kufanya wakabaki kwenye ulimwengu wa michezo.

Ni wachezaji wengi ikiwa hawatafuatiliwa watakuwa nje ya mpango jambo ambalo ni hasara kwa taifa hasa kwa upande wa wale wazawa ambao walikuwa wanafanya vizuri.

Rai yangu ni kwamba wachezaji wasibadilishe maamuzi na kuukacha mpira bado wanapaswa kuendelea kuwa kwenye familia ya mpira kila wakati.

Ilikuwa wazi tangu awali kwamba kuna suala la kushuka hivyo kwa wakati ujao ikiwa watapata timu za kucheza basi wanapaswa wakazane kufanya vizuri mwanzo mwisho.

Imani yangu ni kwamba kwa kuwa TFF wanajua suala hili basi watakuwa wameandaa mazingira rafiki kwa msimu ujao ndani ya Ligi Daraja la Kwanza ili wale ambao watabaki na timu waweze kuwa katika mazingira mazuri.

Kwa Ligi Daraja la Kwanza mambo huwa yanakuwa magumu kwa kuwa kila mmoja anapambana na hali yake. Suala la ukata limekuwa ni wimbo usio na tiba jambo ambalo linapaswa kufanyiwa kazi.

Jambo la msingi kwa timu ambazo zimeshuka ni kutazama makosa ambayo waliyafanya wasiyarudie katika ligi ambayo wanakwenda kushiriki.

Kikubwa kinachohitajika ni maandalizi makini na kila mmoja kutimiza majukumu yake kwa wakati sahihi jambo litakaloongeza ushindani na kuleta matokeo mazuri.

Maboresho yakiwa mazuri katika Ligi Daraja la Kwanza hasa katika usimamizi itaongeza ushindani zaidi kwa timu shiriki.

Kila mmoja na aone kwamba jukumu lake ni kutimiza malengo ya timu ambayo imejiwekea kwa kuwa hakuna jambo ambalo linafanyika bila mpango kazi.

Huku katika Ligi Daraja la Kwanza ni kiwanda cha kutengeneza wachezaji wajao ambao watakuwa tegemeo kwenye timu ya taifa ya Tanzania.

Ikiwa huku ni sehemu ya kiwanda kwa wachezaji basi jambo la msingi ni mazingira mazuri ya utendaji kazi kwao kuboreshewa ili kuongeza nguvu zaidi kwenye ushindani.

Ni moja ya ligi ngumu ambayo ukienda kichwakichwa lazima ukutane na anguko hasa kwa zile timu ambazo zimetoka kushuka msimu huu.

SOMA NA HII  KWA YANGA HII...MHHH..YANI WAKIJAA TU NA KUJISAHAU WAMEKWISHAA MAZIMA..

Muda uliopo ni mdogo kwa ajili ya maandalizi basi na utumike kwa usawa ili kuweza kupata kile kinachostahili kwa mashabiki pamoja na wamiliki wa timu.

Ipo wazi kwamba msimu ujao utakuwa na ushindani mkubwa tofauti na msimu huu ambao nao umechangamka kwa timu kusaka ushindi.

Ukiachana na maandalizi ya timu ambazo zimeshuka daraja pamoja na Ligi Daraja la Kwanza kiujumla tunaona pia ni muhimu kuwekeza nguvu katika maandalizi ya viwanja.


Hili ni eneo muhimu kwa kuwa burudani zote za mpira na kuwajua wachezaji makini zinafanyika hapa muda wote. Tunaona kwamba kwa msimu uliopita viwanja vingi vilikuwa vinakumbana na ile adhabu ya kufungiwa.

Kwa kuwa maandalizi ya msimu ujao yanaanza sasa basi ni muda wa kuweza kuboresha pia na sehemu ya kuchezea. Hii itaongeza ule ushindani pia .


Iwe kwa timu zote shiriki kuanzia Ligi Daraja la Kwanza,Ligi Daraja la Pili mpaka Ligi Kuu Bara hapo nina amini kuna jambo litaonekana.


Kila ambaye anahusika katika usimamizi wa uwanja basi ni jukumu lake kuona kwamba kwa msimu ujao pale ambapo anasimamia panakuwa sehemu bora.


Mazingira ya uwanja yakiwa mazuri yanafanya burudani iwe halisi kutoka kwa wachezaji pamoja na mashabiki kuona kile kilicho bora kwao.


Imani yangu ni kuona kwamba msimu ujao maandalizi yake yanakuwa tofauti kwa kila jambo ili ushindani uwe mkubwa zaidi ya huu ambao ulikamilika.


Ushindani ukiwa mkubwa unafanya wachezaji ambao watapatikana kuwa bora na wenye uwezo mkubwa hasa pale watakapopewa nafasi ya kucheza kwenye timu ya taifa.


Maboresho kwa sehemu ya kuchezea ni muhimu kuanza kwa wakati huu. Ikiwa itakuwa hivyo ushindani utakuwa mkubwa zaidi ya wakati ambao umepita.


Pia kwa wakaguzi ambao wamekuwa wakifanya kazi hiyo kutoka TFF wito wangu ni kuona kwamba kwa muda huu kabla ligi haijaisha wanazikumbusha timu kufanya hivyo.


Ukweli ni kwamba pale ambapo wamilik watakumbushwa na mamlaka husika kuna uzito utaongezeka hasa katika utekelezaji kwa ajili ya msimu mpya.


Kwa wale ambao wameshuka tusiwapotezee pia kwa kuwa bado ni familia ya michezo. Nao pia wakipata nafasi kwa wakati ujao wasipoteze katika maisha yao mapya.