Home news PAMOJA NA CORONA, FAMILIA WAITAJA MECHI YA SIMBA VS YANGA CHANZO CHA...

PAMOJA NA CORONA, FAMILIA WAITAJA MECHI YA SIMBA VS YANGA CHANZO CHA KIFO MWL KASHASHA


KIFO ni fumbo. Hutamsoma tena Mwalimu Alex Kashasha kwenye kolamu yake aliyokuwa akiandika kwenye ukurasa wa 12 wa Mwanaspoti kila Jumamosi. Kifo kimemchukua, atazikwa Dar es Salaam Jumatatu.

Hutasikia tena ile misemo, mbwembwe zake akitangaza mpira kwenye TBC au akifafanua jambo kwenye Mwananchi Digital.

Kaka wa Marehemu, Deus Alexander alisema alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa Uviko-19 ambao aliupata akitoka kwenye mechi ya Simba na Yanga mjini Kigoma baada ya kupiga picha na kila aliyekuwa akimuomba kwenye vituo mbalimbali akiwa kwenye basi kurejea Dar.

Alisema watamzika Jumatatu ya Agosti 23 katika makaburi ya Kinondoni jijini Dar es Salaam mchana.

“Kwa kuwa mdogo wangu alikuwa mtu wa watu hatutaki kuwanyima mashabiki na wanasoka wenzake uhuru, hivyo tunatafuta eneo la wazi ambalo litakuwa rahisi kumuaga na tutawaambia mapema,kumuaga itakuwa Jumapili, kiukweli tuna maumivu kumpoteza mtu mwenye upendo sana kwenye familia,” alisema na kuongeza Kashasha alianza kuumwa tangu alipotoka kwenye fainali za Kombe la ASFC mjini Kigoma Julai 25.

“Alikuwa anasumbuliwa na figo ndani ya miaka miwili ambayo alikuwa anahudhuria kliniki, tatizo lilipoanzia alitoka na basi kutoka kwenye fainali ya Simba na Yanga, kitendo cha kupiga picha na watu kila kituo kulimfanya apate ugonjwa wa Uviko 19 kwani alifika nyumbani akiwa amechoka sana,” alisema kaka yake na kuongeza ilimletea shida, alifika amechoka sana.”

“Hospitali wakamtibia ugonjwa wa mapafu lakini baada ya kuona hali bado haipo vizuri wakamfanyia upasuaji wa kusafisha figo, baadaye Mungu akamchukua,” alisema.

Kashasha ameacha mkewe Elizabeth Sawe na watoto wawili Theopster Kashasha (25) na Theonester Kashasha (16).

Alisema ndugu zao wote wako Dar es Salaam wakiwemo shangazi zake ambao walikuja kwenye harusi ya mtoto wa mdogo wa marehemu ambaye harusi yake ilitarajiwa kufanyika leo Dar es Salaam.

“Sisi tulishafanya sendoff wiki mbili zilizopita na kesho (leo) ndiyo harusi hivyo ndugu wote wako hapa mjini ndio maana tumeamua kumzika hapa hapa mjini Kwa kuwa hata wazazi wetu walishatangulia mbele za haki,” alisema.

SOMA NA HII  MTAZAMO WA EDO KUMWEMBE KUHUSU TUHUMA ZA MASHABIKI JUU YA UWEZO WA JOHN BOCCO...

Mhariri Mkuu wa Michezo wa Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC), Enock Bwigane aliliambia Mwanaspoti jana kwamba; “Kwa namna ambavyo alikuwa anazungumza sikutarajia leo hii kutokuwa naye, maana alitaka kujua usajili unavyoendelea, ligi ijayo kama haitakuwa na viporo, kiukweli alitarajia kufanya mengi msimu ujao.

“Alikuwa baba, mwalimu, babu, hakuwa mnafiki kuelekeza ukweli iwe jambo limeenda vizuri au vibaya, alipenda vijana wajifunze, alitengeneza umoja wa kazi, ndio maana yalitokea maneno maarufu kama kwako Mwalimu Kashasha,” alisema.

Kipa wa Taifa Stars, Metacha Mnata alisema anakumbuka msimu wa 2019/20 wakati walipokwenda kucheza mechi dhidi ya Coastal Union ya Tanga, alimfuata na kumwambia abadilike baadhi ya maeneo ili aweze kufika mbali.