Home Makala SIMBA, YANGA JIKITENI KWENYE ISHU YA KIBIASHARA, POROJO MUDA WAKE UMEISHA

SIMBA, YANGA JIKITENI KWENYE ISHU YA KIBIASHARA, POROJO MUDA WAKE UMEISHA


KWA miaka mingi kilio cha wadau na mashabiki wengi wa timu za Simba na Yanga kimekuwa ni kuona timu hizi kongwe zaidi nchini na zenye historia ya kipekee zikitoka kwenye kuendeshwa na porojo hadi kuendeshwa kibiashara zaidi.

Ilikuwa inatia ukakasi na aibu pia kuona Simba na Yanga zinaendeshwa kwa bakuli, huku nje zikijinasibu ni moja ya timu kubwa na zenye historia ya kipekee nchini.

Kwa miaka ya hivi karibuni tumeanza kuona ule uswahili kwenye hizi klabu ukianza kutoweka kidogo kidogo baada ya watu wenye nia ya dhati ya kuzibadilisha timu hizi kutoka kwenye kuendeshwa kimazoea hadi kuendeshwa kibiashara.

Leo nilitarajia kuona tayari Simba na Yanga zimeshatambulisha jezi zao kuelekea msimu mpya wa Ligi Ku Bara, kungekuwa na jezi ya Fiston Mayele, Makambo, Diarra, Djuma Shabani na wachezaji wengine ambao tayari wamesajiliwa Yanga.

Kwa upande wa Simba nilitarajia kuona jezi ya Peter Banda tayari ikiwa sokoni hii ingezidi kuongeza mapato kwenye klabu hizi kuliko kuzindua jezi za msimu wakati ligi ikiendelea.

Moja ya mambo ya kupongezwa kuona sasa hivi timu hizi zimesheheni watu ambao wanafikiri nje ya boksi ili kuzinufaisha timu hizi tofauti na zamani lakini jitihada za ziada zinahitajika katika kutanua mifuko ya timu hizi ili ziweze kujiendesha zenyewe bila kutegemea hisani ya wadau.

Ukipiga hesabu idadi ya mashabiki wa Simba na Yanga nchi nzima ni wazi wameteka zaidi ya asilimia themanini ya mashabiki wote wa soka nchini hivyo timu hizi zinatakiwa kugeuza mtaji wa mashabiki wao kama sehemu ya kuiinua timu kiuchumi.

Hapa unaweza kupiga hesabu za harakaharaka kama Simba ingekuwa tayari imetambulisha jezi za msimu na jezi ya Banda iko sokoni kwa bei ya chini tu shilingi elfu 35 na ikanunuliwa na mashabiki elfu hamsini, Simba ingekuwa na nafasi ya kuingiza zaidi ya shilingi milioni 175, hiyo ni kwa jezi ya mchezaji mmoja tu.

Yanga pia kupitia mauzo ya jezi ya Mayele, Makambo na Ukonde pia ingenufaika sehemu kubwa kupitia mauzo ya jezi za wachezaji tu. Tumeshuhudia kwa wenzetu mauzo ya jezi pekee yanarudisha gharama zote za mchezaji hivyo inapaswa na timu zetu kuanza kuingia kwenye mifumo ya aina hiyo.

SOMA NA HII  WAWAKILISHI WETU KIMATAIFA WAJIPANGE SAWASAWA

Tungetarajia kuona vitabu (notebook), mabegi, skafu, kalamu na vifaa vingine vyenye nembo ya klabu zenu na picha za wachezaji wenu kama sehemu ya mapato ya ziada kwenye timu zenu.

Wadau wengi wanatamani kuona ushindani wenu ukijikita zaidi kwenye kuinua uchumi wa klabu zenu na si kuendekeza porojo ambazo hazina manufaa yoyote kwa ustawi wa timu zenu.

Wengi wanatamani kuona Simba, Yanga na hata Azam zikiingia levo za TP Mazembe, Al Ahly na hata zikipiga hatua kubwa zaidi na si kujikita kwenye mambo ambayo hayana tija kwenye klabu zenu.

Wengi wanatarajia mambo makubwa zaidi ndani ya timu zenu isiishie kwenye Super Cup na Yanga Marathon pekee bali mjikite katika kubuni na kuanzisha vyanzo vingi vya mapato ambavyo vinaweza kuzibadilisha timu hizi na kumudu kujiendesha zenyewe na kuachana na masuala ya bakuli na changia changia.

Ushindani wenu uwe ni wenye kuleta faida kwenye timu zenu na si kutaka kuvurugana na kuanzisha uhasama ambao hauna faida yoyote kwa mustakabali mpana wa klabu zenu. Ili muweze kufika levo za juu kama timu kubwa Afrika ni lazima mjikite kwenye ushindani wa kibiashara zaidi na si porojo.

Nilitarajia wakati Simba wanamtambulisha Bernard Morrison tayari wangekuja na data za mauzo ya jezi ya kiungo huyo mwenye ushawishi mkubwa kwa mashabiki wa soka nchini kutokana na vituko vyake vya ndani na nje ya uwanja ambavyo vimekuwa kivutio kikubwa kwa mashabiki wake.

Ni lazima mkubali kuendana na mabadiliko ya kimazingira kwani hivi sasa soka ni Biashara ambayo inaingiza fedha nyingi ndiyo maana Azam hawakusita kuweka udhamini mnono wa zaidi ya shilingi bilioni 225 kudhamini Ligi Kuu Bara.