CLIFORD Ndimbo, Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania, (TFF) amewaomba Watanzania kuzidi kuiombea dua Tanzania na kuendelea kuifuatilia bila kuchoka ili iweze kufikia malengo na kutimiza majukumu ya kupeperusha bendera.
Leo Septemba 2, Stars inayonolewa na Kocha Mkuu, Kim Poulsen ina jukumu la kusaka ushindi kwenye mchezo wa kufuzu Kombe la Dunia na itakuwa ni dhidi ya DR Congo, nchini Congo.
Mchezo huo unatarajiwa kuchezwa majira ya saa 10:00 jioni kwa saa za Afrika Mashariki itakuwa ni kwenye Uwanja wa TP Mazembe uliopo Lubumbashi, DR Congo.
Akizungumza na Saleh Jembe, Ndimbo amesema kuwa leo ni siku muhimu kwa Stars kusaka ushindi na mchezo utakuwa na ushindani kwa kuwa hata wapinzani wao pia wanahitaji ushindi.
“Watanzania waendelee kuiombea dua Stars leo Alhamisi itakuwa na mchezo dhidi ya DR Congo ambao utachezwa nchini DR Congo kwa sababu ni timu yetu na inatuwakilisha wote.
“Dua ni muhimu na waendelee kuwa nayo bega kwa bega kwa sababu wamekuwa wakifanya hivyo siku zote na kila wakati hivyo inabidi waendelee.
“Wakimaliza hapo watakuwa na mchezo mwingine pia muhimu hivyo bado kuna kazi ya kufanya na imani yetu ni kuona kwamba matokeo yanapatikana,” amesema.
Katika kufuzu Kombe la Dunia 2022 nchini Qatar Taifa Stars ipo kundi J ikiwa pamoja na DR Congo, Madagascar na Benin.