IKO wazi. Ubora wa Simba na Namungo kwenye michuano ya kimataifa msimu uliopita umeipa heshima Tanzania. Imepewa uwakilishi wa timu nne msimu huu kwenye Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho.
Ni heshima ya aina yake ambayo kwa namna yoyote ile inapaswa kulindwa na washiriki wa msimu huu kwa maana ya Yanga wenyewe kwenye Ligi ya Mabingwa na Azam, Biashara katika Shirikisho.
Kila mmoja anapaswa kupambana ndani ya uwanja na lengo la kwanza liwe kufika hatua ya makundi ya michuano hiyo ndipo malengo mengine yafuate. Yanga haijashiriki michuano hiyo kwa misimu minne sasa.
Na katika wawakilishi wa Tanzania yenyewe ndiyo imefanya usajili mkubwa zaidi na matarajio ya mashabiki wao ni makubwa zaidi. Wanawajua wachezaji wao kwa sura na rekodi zao za timu walizotoka haswa wale wa DR Congo hivyo ni mtihani mkubwa uliopo mikononi mwa Kocha Mohammed Nabi kutengeneza timu ya ushindani.
Kwasasa walivyo Yanga wana wachezaji lakini hawana timu ya ushindani. Wana siku zisizozidi tisa kujiweka sawa kabla ya kuwakabili Rivers United ya Nigeria kwenye mchezo wao wa kwanza Septemba 12 Jijini Dar es Salaam na kurudiana Septemba 19 ugenini.
Hii ni mechi ngumu ambayo Yanga wanapaswa kuiangalia kwa jicho la pili. Wakiibeza timu hii kwa kuangalia jina lao na rekodi zao wataadhirika kweupe. Yanga wanapaswa kujiandaa siriazi kwelikweli maalum kwa mchezo huo wakati wakiendelea kujipanga kivingine. Wakijaa upepo tu wakashindwa kuumaliza mchezo huo itawavurugia msimu mzima kwavile baada ya hapo wataingia kwenye ngao ya jamii na watani zao kabla ya kuanza msimu.
Ni wazi kwamba kiufundi Yanga bado sana na wanahitaji muda usiopungua siku 60 kupata timu ya ushindani, lakini ndani ya mazingira hayohayo wanapaswa kufanya kitu kimataifa kuonyesha thamani yao na kuthibitisha kwamba hawajabebwa bali wana uwezo.
Kosa walilofanya Yanga la kwanza ni kwenda kambini nchini Morocco bila kufanya tathmini ya kutosha ndani na nje ya uwanja. Sawa kubadilisha mazingira ni muhimu kisaikolojia lakini kwa upya wa timu waliyonayo hakukuwa na ulazima sana haswa kwa kuzingatia wana kambi nzuri ya kisasa iliyopo Kigamboni.
Muda waliopoteza angani, kuuguza baadhi ya wachezaji wao ungetosha kabisa kufanya maandalizi ya maana pale Kigamboni na timu ingekuwa kwenye kiwango kizuri zaidi ya kile kidogo kilichoonekana dhidi ya Zanaco kwenye Uwanja wa Mkapa ile siku ya Mwananchi. Kambi ya Morocco imewagharimu zaidi kiufundi kwani sasa hata baadhi ya mastaa wao wamekwenda kwenye timu za Taifa hata hawajajuana sura na wenzao, achilia mbali kiufundi.
Kwahiyo mnaeza kuona mzigo Yanga walionao. Ndio maana nasisitiza kwamba hizi kambi za nje ni nzuri lakini timu zilizoendelea huwa zinafanya tathmini ya kutosha ya mazingira ya ndani na nje ya uwanja kabla ya kwenda huko. Vinginevyo ndiyo hivyo unakuta timu inaingia hasara kwa kutumia fedha nyingi lakini vilevile wachezaji wanaishia kupiga selfi tu. Tujitafakari.
IMEANDIKWA NA DOTTO JONGWE (wakuja@gmail.com)