UONGOZI wa Yanga umebainisha kuwa kukosekana kwa vibali kwa wachezaji wao watatu sio makosa ya Yanga bali kuna sababu ambazo zilitokea zikasababisha suala hilo.
Nyota huyo ni Khalid Aucho, Fiston Mayele na Djuma Shaban hawatakuwa sehemu ya kikosi kitakachomenyana na Rivers United unaotarajiwa kuchezwa Uwanja wa Mkapa, Septemba 12.
Haji Manara, Ofisa Habari wa Yanga amesena kuwa:”Kukosekana kwa wachezaji hawa haikuwa makosa ya Yanga, Mayele na Djuma Shaban mikataba yao ilikuwa inaisha tarehe 31.
“Sisi tulipeleka maombi ya ITC Congo mara baada ya kukamilisha usajili wa wachezaji hawa ila walituambia kwamba tusubiri kwanza mpaka mikataba yao iishe, kukawa na mvutano mkubwa.
“Tukasema inawezekana vipi hilo wakati dirisha la usajili linafungwa Agosti 31, wakatoa siku moja baada ya dirisha kufungwa na kilichotokea Caf kwa mujibu wa taratibu zao wakasema muda umekwisha.
“Hivyohivyo kwa Khalid Aucho, kulikuwa na mgogoro mkubwa na klabu yake hakulipwa kwa muda mrefu baadaye mgogoro ulikwenda Fifa wakasema ni mchezaji huru ila baadaye ikawa shida kupata ITC yake na watu wa Misri wakasema kwamba tumechelewa.
“Bado tunaendelea kupambana kwa ajili ya kuona tunapata ITC zao na kwa kuwa muda bado upo mashabiki watulie wasiwe na wasiwasi,” amesema Manara.