Home Makala NI MANARA DHIDI YA MANARA,TEKNOLOJIA IMESIMAMA KATIKATI

NI MANARA DHIDI YA MANARA,TEKNOLOJIA IMESIMAMA KATIKATI


KUPITIA teknolojia hakuna tena ambacho 
unaweza kukifanya siri zaidi ya kuyafanya mambo yaende kwa njia sahihi.

Teknolojia inakua na kuimarika kwa haraka sana hadi kufikia kutulazimisha kuongeza umakini kwa asilimia 100 kwa kila tunalolifanya leo.

Hali ilivyo ni hivi; kuna uhusiano mkubwa sana kati ya kile unachokisema leo na utakachokizungumza kesho. Vinaweza kuwa na muunganiko mkubwa na wa karibu sana na hii yote ni kuhusiana na suala la teknolojia.

Kasi ya ukuaji wa teknolojia umeifanya dunia kuwa kijiji, acha tu katika mawasiliano ya kawaida lakini imehamia hadi katika mawasiliano ya mazungumzo kwa kuwa si suala la upigaji simu pekee, badala yake unaweza kuwasiliana na mtu mwingine kupitia Whatsapp na application nyingine kibao kama nyenzo ya mawasiliano.


Kadiri siku zinavyosonga, suala la sauti ambalo lilionekana liko juu zaidi linakwenda kuzidiwa nguvu na suala la sauti na mwonekano kwa maana ya video.

Video ndio zinazoaminika zaidi, kwamba anazungumza anasikika na anaonekana.Ushahidi wa video unachukua uaminifu mkubwa kwa wahusika wanaokuwa wanazungumzia jambo fulani.

Ndio maana umeona suala la mjadala ulioanzishwa na Haji Manara, msemaji wa Yanga ukiisha haraka sana kwa kuwa teknolojia imemhukumu.

Teknolojia imemhukumu Manara kupitia yeye mwenyewe. Hakuna yoyote katikati yake ameweka maneno. Zaidi amezungumza yeye na akajijibu yeye.

Mjadala aliouamsha ni kwamba Yanga ndio klabu yenye makombe mengi zaidi iliyoshinda katika michuano mbalimbali.

Wakati anayasema hayo, tayari yalikuwa yanapingwa na wadau wengi wa mpira ambao wanajua Simba ndio ina makombe mengi.

Wadau hao wamekuwa na sehemu nyingine ya uthibitisho ingawa, uthibitisho wa uhakika zaidi wao wameutumia ni wa Manara mwenyewe. Maneno ambayo aliyazungumza miezi kadhaa tu iliyopita.

Katika hauli hiyo, Manara wakati akihojiwa na Baruan Muhuza wa Azam TV alisema kwamba Simba ndio yenye makombe mengi zaidi akijaribu kutoa ufafanuzi kadhaa.

Bahati nzuri sana, hakuna aliyempinga wakati ule kwa kuwa limekuwa ni jambo lililokuwa likijulikana licha ya kuwepo na mkinzano wa idadi sahihi ya Simba kachukua mangapi na Yanga anayo mangapi.

SOMA NA HII  BAADA YA KUIONA SIMBA ILIVYOCHEZWA BOTSWANA..EDO KUMWEMBE AGUNA KISHA AFUNGUKA HAYA


Safari hii kungeweza kuwa na ubishi mkubwa, kwa kuwa Manara amezungumza kitu tofauti na kinachofahamika lakini bahati mbaya zaidi, teknolojia inakwenda kuwa kigezo cha kumrudisha nyuma katika kauli yake hiyo.


Bahati mbaya zaidi, anayetumika kumzima Manara kutokana na alichokisema ni Manara mwenyewe. Kwamba Simba ndio kubwa zaidi kama ukisema suala la makombe mengi zaidi iliyobeba.


Video ya Manara akisema Yanga ndio ina makombe mengi zaidi na Simba ina makombe mengi zaidi, zimeunganishwa.

Zote anaonekana na kusikika Manara akisema, hakuna mtu mtu mwingine.Kunakuwa hakuna ubishi kwa kuwa anayezungumza ni Manara na anayemjibu ni Manara. Haya yote ndio sehemu ya kuonyesha kiasi gani teknolojia inapiga hatua kwa kasi kubwa.


Unaweza kusema kama ni ubishi, wanaobishana ni akina Manara na Manara mmoja anampinga mwingine. Lakini haya yote ni kutokana na namna teknolojia ilivyopiga hatua.


Achana na yale mambo ya kishabiki, hapa piga hesabu ya teknolojia yenyewe na ujue inatufundisha mambo mengi sana hasa kwa wale wenye uwezo wa kufanya jambo au mambo mbele ya jamii.


Kwamba siku zijazo zinaweza kushikiliwa na zile zilizopita kulingana naulichokizungumza. Hivyo ni vizuri sana kuwa makini maradufu kwa kila unachokizungumza leo.

Kama hautakuwa makini, hakutakuwa na mtu mwingine, badala yake wewe mwenyewe kupitia teknolojia utakinzana na wewe mwenyewe na mwisho utashindwa na wewe mwenyewe.


Ndio maana nikasema kilichotokea kuanzia jana kuhusiana na alichokisema Manara na baadaye kujibiwa na alichowahi kukisema,maana yake ni funzo ambalo hatupaswi kuona limemtokea Manara tu. 

Badala yake hata wewe na mimi kama tunachozungumza hatutakuwa nacho makini, kitatuangusha katika siku za usoni.


Saleh Ally