YANGA wametamba kwamba mechi yao ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Rivers United ya Nigeria wataimalizia jijini Dar es Salaam, Jumapili.
Bilionea wa klabu hiyo, Gharib Said na jopo la Yanga wamesisitiza hata mechi ya marudiano nchini Nigeria tayari wameshamaliza mkakati wake, hivyo mashabiki wategemee kishindo kinakuja katika Uwanja wa Mkapa.
Habari njema zaidi ni kwamba watakodi dege la kuwapeleka na kuwarudisha Nigeria ili kuondoa figisu zinazoweza kutokea.
Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Yanga, Rodgers Gumbo amesema kuwa kila kitu kipo sawa kuelekea mchezo huo na sasa wanawasubiri wapinzani wao tu wafike wamalizane nao ili warejee kimataifa kibabe kwelikweli.
Gumbo alisema hawana wasiwasi na maandalizi ya kikosi chao ambapo katika mipango yao muhimu ni kwamba wanataka kuona Rivers wanamalizwa katika mchezo wa hapa nyumbani kabla ya ule wa marudiano.
“Tumejiandaa vizuri wala hatuna wasiwasi, tumeangalia pia maandalizi ya kiufundi ya timu yetu. Watu hawatakiwi kupata wasiwasi kikosi kimeandaliwa vyema,” alisema Gumbo ambaye amedumu katika kamati hiyo kwenye utawala wa Dk Mshindo Msola.
“Tunajua hizi mechi ni ngumu, lakini Yanga haijajiandaa kwa unyonge. Tupo tayari katika mikakati ya kushinda hasa hii mechi ya hapa nyumbani na sio kwa kubahatisha tunachotaka, ni kuona hizi mechi mbili tunamaliza kazi kubwa hapa nyumbani.
“Tunataka kushinda kwa ushindi mzuri usio na mashaka hapa nyumbani. Ni muhimu katika mechi za namna hii ukawa na faida ya kuweza kutumia hatua ya kuanzia nyumbani ili kule kwao usiwe na kazi ngumu na hiki ndicho Yanga itakachofanya.
“Kila mchezaji ambaye alikuwa nje wameshafika, tuliandaa mpango maalumu wa kuhakikisha kila mmoja anawahi hii mechi na maandalizi ya mwishomwisho ambayo ni muhimu kwa timu na kazi yetu kama kamati tumeikamilisha.”
Msemaji wa Klabu ya Yanga, Haji Manara alisisitiza jijini Dar es Salaam jana kwamba kaulimbiu kwa ajili ya mechi hiyo ni “The return of champions” akimaanisha kurejea kwa mabingwa.
Manara aliongeza kwamba malengo yao ya msimu huu ni kuvuka hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, kutwaa ngao ya jamii, Kombe la Mapinduzi, FA na Ligi Kuu Bara na kwamba hawaachi kitu chochote, huku akikiri kutokuwapo kwa Khalid Aucho, Fiston Mayele na Djuma Shabaan kwenye mechi ya Jumapili kutokana na vibali vyao kuchelewa.
Aliwataka mashabiki pia kujitokeza kwa kuwa watapambana kuhakikisha wachezaji wanawapa ushindi kwani wana kikosi kipana na hawaingii Kwa Mkapa kinyonge.
BILIONEA ACHUKUA AIRBUS
Wakati Gumbo na kamati yake yenye vigogo tisa wakijipanga hivyo, nyumbani Bilionea wao, Gharib Mohamed hesabu zake zimeshahamia katika mechi ya marudiano na mpaka jana alikuwa katika hatua za mwisho za kukodi ruti ya dege kubwa.
Anachotaka kufanya Gharib ni kuchukua ndege kubwa ya Shirika la Tanzania aina ya airbus ambayo itawapeleka Yanga na timu yao nzima nchini Nigeria, kisha baada ya mchezo tu kumalizika wageuze nayo.
Hesabu kubwa za kuchukua ndege hiyo ni kwamba vigogo wa kamati ya mashindano na bilionea huyo wameshtukia kuwa mchezo wa marudiano unaweza kupelekwa sehemu ambayo wanaweza kutakiwa kuunganisha ndege nyingi hatua ambayo itawachosha wachezaji.
“Ukichukua ndege hizi za kibiashara utahitajika kupoteza siku nyingi njiani na mbaya zaidi unaweza kukuta kule Nigeria mkapelekwa sehemu ngumu zaidi ambayo itahitajika mchukue ndege nyingine, sasa Gharib na wenzake wameona ni bora wachukue ndege maalumu tu kutoka hapa,” alisema mmoja wa vigogo wa Yanga.
“Hiyo ndege itaondoka moja kwa moja mpaka mji ambao mchezo utafanyika na haitaondoka, itasubiri timu icheze na mechi ikiisha inarejea haraka nchini kuendelea na mambo mengine.”
Yanga imejipanga kuvuka hatua ya awali ambayo inaamini baada ya hapo wachezaji wao watakuwa wameshakuwa fiti kimchezo na wana uelewano mzuri.