JESHI la Yanga linatarajiwa kupaa usiku wa leo kwenda Nigeria, huku kocha wao wa zamani, Mwinyi Zahera akimaliza mechi ya marudiano mjini Port Harcourt kibabe kwa kutoa ramani ya kumaliza mchezo mapema kwa Kocha Mkuu, Nasreddine Nabi.
Aidha Zahera ametoa msimamo wake kwa wana Jangwani kwa kusema kuwa, kocha Nabi bado ni mtu sahihi ndani ya kikosi cha Yanga na kwamba apewe muda, lakini kuelekea mchezo wa marudiano akampa mambo matatu ambayo kama watafanya sawa basi watapindua meza.
Kocha Zahera ambaye aliiangalia mchezo wa kwanza hapa jijini Dar es Salaam Yanga ikilala kwa bao 1-0 dhidi ya Rivers United jamaa amesema bado timu yake hiyo ya zamani ina nafasi ya kupindua meza.
Zahera amesema kwamba Yanga kitu cha kwanza ambacho Nabi anatakiwa kukifanya ni kupanga vizuri safu yake ya kiungo na ile ya ulinzi isiruhusu bao lolote la mapema ndani ya dakika 20 za kwanza.
“Walifanya makosa katika safu ya ulinzi hawakuwa wanaruka na walifanya makosa mengi, ile haitakiwi kufanyika kule kabisa wanatakiwa kuwa imara na kucheza na nidhamu kubwa ya mchezo,” alisema Zahera na kuongeza;
“Wanatakiwa kutulia wakicheza vizuri nyuma itawashtua wale wapinzani wao na wao wataanza kuona mchezo unakuwa mgumu na hapo kama wataweza kufikisha mpaka dakika 20 au 30 hawajaruhusu bao hiyo itakuwa ni jambo zuri kwa Yanga.”
Zahera alisema katika dakika 25 za kwanza Rivers watashambulia wakitaka kupata bao ambapo Yanga haitatakuiwa kujilinda lakini wanatakiwa kutumia mashambulizi ya kushtukiza kusaka bao la kwanza.
“Sina maana kwamba Yanga icheze kwa kujilinda wanatakiwa kukaba kwa nidhamu lakini wapinzani wao watakuja kusaka bao na Yanga sasa wanatakiwa kufanya mashambulizi mazuri ya haraka ya kushtukiza.
Kocha huyo Mkongomani aliongeza kwamba jambo la tatu ni kwamba kila mchezaji wa Yanga atakayepata nafasi ya kufunga anatakiwa kutambua jinsi walivyowaangusha mashabiki wao katika mchezo wa nyumbani akiwataka kutulia na kufunga.
“Mashabiki wa hapa waliumia na yale matokeo Yanga ilitengeneza nafasi nyingi ila wachezaji wanatakiwa kutambua kwamba wanatakiwa kuwatuliza mashabiki wao kwa kutulia na kufunga.
“Hakuna mchezo ambao unakosa kutengeneza nafasi yapo makosa Rivers watayafanya wachezaji wa Yanga wanatakiwa katika mchezo ujao wasahihishe makosa kwa kutumia nafasi itakuwa ni aibu Yanga kutolewa hatua ya awali.
Yanga inaondoka leo Ijumaa saa 2 usiku kuelekea nchini Nigeria tayari kwa mchezo huo wa marudiano wakitumia ndege ya shirika la Tanzania itakayopeleka na kuwasubiri kisha kurejea nayo.
Katika mchezo wao wa kwanza uliopigwa wikiendi iliyopita, Yanga ililala kwa bao 1-0 na mechi yao ya marudiano inahitajika kushinda si chini ya mabao 2-0 ili kutinga raundi ya kwanza ambapo huenda ikakutana na Fasil Ketema ya Ethiopia au Al-Hilal Omdurman ya Sudan ambao katika mechi yao ya kwanza zilitoksa sare ya 2-2 mjini Addis Ababa.