NI kesho Septemba 25 ambayo itakuwa ni Jumamosi, pazia la Ligi Kuu Tanzania Bara litakuwa linafunguliwa kwa mchezo wa Ngao ya Jamii kuchezwa.
Kawaida ufunguzi huo huzikutanisha timu mbili, moja bingwa wa ligi na ile ya pili huwa ni bingwa wa FA.
Msimu uliopita wa 2020/21 Simba ilifanikiwa kuchukua makombe yote mawili na Yanga ilimaliza nafasi ya pili kwenye michuano hiyo. Simba walicheza fainali ya FA na Yanga, hivyo kanuni ikaeleza moja kwa moja kuwa timu hizo zitakutana kwenye mchezo wa Ngao ya Jamii.
Uwepo wa kanuni hiyo imetufanya tushuhudie rekodi mpya kwenye soka la Bongo, kwani miamba miwili ya soka nchini inakwenda kukutana kwa mara ya nne ndani ya mwaka mmoja.
Ni mara chache sana kutokea jambo hili ndani ya mwaka mmoja, ingawa dalili zilionyesha uwepo wa rekodi hii toka msimu wa 2019-20, walipokutana mara tatu.
Walicheza mechi mbili za ligi na mechi moja ya Kombe la FA, Simba wakiwachapa 4-1 Yanga, mchezo ulichezwa Uwanja wa Mkapa hatua ya nusu fainali.
Kabla ya hapo mara ya mwisho timu hizi kucheza mechi zaidi ya mbili ilikuwa ni wakati wa mechi za Nani Mtani Jembe ambazo zilifanyika misimu miwili mfululizo.
Mwaka 2013-14, Yanga wakichapwa 3-1 na msimu wa 2014-15 Yanga wakilala tena kwa mabao 2-0. Mechi ambayo ilimfukuzisha kazi aliyekuwa kocha wa timu hiyo Marcio Maximo.
Maximo ana hadithi tamu na ya kuvutia kwenye soka la Tanzania wakati akiwa kocha wa Taifa Stars, akitajwa kama kocha aliyetengeneza hamasa kwa Watanzania ambayo imedumu hadi leo.
Turudi sasa kwenye hoja ya leo ambayo ni kukupitisha katika mechi tatu zilizopita ambazo miamba hii imecheza kwa mwaka 2021 kabla ya mechi ya nne kupigwa.
Mechi hiyo ijayo inatarajiwa kuwa ya aina yake kutokana na mabadiliko ya vikosi vyote viwili, kwani kila timu imefanya usajili wa maana.
Chagizo lingine kubwa, ni matokeo ya timu hizo kwenye mechi zao zilizochezwa wikiendi iliyopita. Simba walichapwa 1-0 na TP Mazembe kwenye kilele cha Simba Day.
Wakati Yanga walichapwa 1-0 na Rivers na kutupwa nje kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika. Hivyo kwa matokeo hayo achilia mbali asili ya mechi yenyewe.
Mashabiki wanatarajia kushuhudia kandanda ya juu sana. Hizi hapa chini ni mechi ambazo miamba hiyo imekutana kwa mwaka huu.
Yanga 4-3 Simba
Idadi ya mabao isikutishe, hiyo ilikuwa ni mikwaju ya penalti baada ya Yanga na Simba kwenda suluhu kwenye dakika za kawaida kwenye fainali ya Kombe la Mapinduzi Cup.
Mchezo ulipigwa Januari 13,Uwanja wa Aman mjini Unguja, Zanzibar. Kocha wa Yanga alikuwa Cedric Kaze na kwa Simba alisimama Suleiman Matola. Yanga wakawa mabingwa.
Yanga 1-0 Simba
Kilikuwa kipigo cha pili kwa mwaka huu kwa Simba. Mchezo huu ulichezwa Julai 3, Uwanja wa Mkapa Dar, kocha akiwa Nasreddine Mohamed Nabi na kwa Simba akiwa Didier Gomes.
Alikuwa ni Zawadi Mauya aliyepeleka kilio Simba, akifunga bao kwa shuti ambalo lilimgonga Shomari Kapombe na kumpoteza Aishi Salumu Manula.
Mmoja wa watu walioshuhudia kipigo hiki cha Simba ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.
Ikiwa ni rekodi nyingine kwa Simba kufungwa na Yanga mara mbili mfululizo mbele ya macho ya Rais wa Tanzania. Ilianzia kwa Hayati John Magufuli, Machi 8, 2020 Bernard Morrison alipiga pigo huru na kuweka mpira kwenye kamba.
Simba 1-0 Yanga
Mchezo ulichezwa Julai 25 Uwanja wa CCM Lake Tanganyika Kigoma, ikiwa ni fainali ya Kombe la Azam Sports Federation Cup au FA.
Simba walifanikiwa kuwa mabingwa kwa ushindi wa bao 1-0, bao lilifungwa na Taddeo Lwanga dakika ya 79 ya mchezo akiunganisha mpira wa kona iliyochongwa na Jose Luis Miquissone.
Ulikuwa mchezo mgumu kwa pande zote mbili na Yanga wakimaliza wakiwa pungufu uwanjani kufuatia kadi nyekundu ya Mukoko Tonombe baada ya kucheza ndivyo sivyo dhidi ya John Bocco.
Septemba 25 nani kuwa mbabe?
Ni swali ambalo majibu yake yatapatikana Jumamosi hii kwenye Uwanja wa Mkapa. Mchezo ambao utakuwa wa kisasi, kusaka heshima na rekodi.