NASREDDINE Nabi, Kocha Mkuu wa Yanga amebainisha kuwa jambo ambalo litachukua muda kwa kikosi hicho kufanya vizuri kwenye mashindano yake yote ni kukosa muunganiko jambo ambalo analifikiria kwa wakati huu.
Katika mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya Simba ni Fiston Mayele alipeleka kilio Msimbazi baada ya kufunga bao mapema dakika ya 10 na Simba walikwama kuweka mzani sawa jambo lililosababisha Ngao ya Jamii kuwa mali ya Yanga.
Akizungumza na Championi Jumatatu, Nabi raia wa Tunisia aliweka wazi kwamba wachezaji waliosajiliwa wana uzoefu mkubwa lakini bado hawachezi wakiwa kama timu.
“Usajili tu hapo siwezi kudanganya ni usajili mzuri umefanywa na viongozi na mimi nimehusika kwa kuwa nipo kwenye kamati ya usajili lakini suala la muunganiko hilo bado halijawa sawa.
“Nikiwa ni mwalimu wa mpira ambaye ninapenda kuona matokeo ninaweka wazi kuwa itachukua zaidi ya wiki mbili na pengine zaidi ya hapo lakini haina maana kwamba tutashindwa kushinda hapana tutafanya vizuri na kila kitu kitakuwa sawa,” alisema Nabi.
Yanga kwa sasa ipo kwenye maadalizi ya mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Kagera Sugar unaotarajiwa kuchezwa Uwanja wa Kaitaba.
Itakuwa ni Septemba 29 ambapo utakuwa mchezo wa kwanza wa ligi kwa timu hizo mbili kwa msimu wa 2021/22.