KOCHA wa Simba, Didier Gomes amesema kuwa Yanga walistahili kushinda mechi ya Ngao ya Jamii kwa sababu walitengeneza nafasi moja na wakaitumia tofauti na wao, huku akisifu usajili wao.
Simba walipoteza kwa kuchapwa bao 1-0 na Yanga kwenye mchezo mkali uliopigwa kwenye Uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam.
Yanga walijipatia bao lao kupitia Fiston Mayele dakika ya 11 baada ya kupata pasi safi kutoka kwa Farid Mussa.
Gomes alifunguka kuwa, kwenye mchezo wowote ambao kombe linakuwa mbele ni lazima timu moja ishinde na nyingine ipoteze na bahati mbaya haikuwa siku yao, Yanga wakashinda mchezo.
“Nawapongeza wachezaji wangu walicheza vizuri, lakini Yanga walipata nafasi na wakaitumia.
“Wamefanya usajili mzuri na wanatimu nzuri sana msimu huu, tunakwenda kujipanga na ligi kwa kuwa tunafahamu kuwa itakuwa ngumu,” alisema kocha huyo.
Gomes ameingia kwenye orodha ya makocha ambao wamepoteza mechi mbili kati ya tatu za Simba na Yanga ambazo zimechezwa ndani ya mwaka mmoja akiwa kama kocha mkuu.
Ilikuwa ni Septemba 25, Uwanja wa Mkapa mchezo wa Ngao ya Jamii ulichezwa na mashabiki wa Yanga kusepa na furaha.
Kwa sasa tayari Ligi Kuu Bara imeanza ikiwa ni mwendo wa mzunguko wa pili baada ya ule wa kwanza kukamilika na Simba wakiwa ni mabingwa watetezi.