MZUNGUKO wa kwanza umekamilika kwa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2021/22 huku rekodi zikiandikwa katika mechi ambazo zimechezwa kwenye viwanja nane tofauti.
Pazia la Ligi Kuu Bara lilifunguliwa Septemba 27 ambapo ilishuhudiwa michezo mitatu ya kukata na shoka ndani ya ligi ambayo imekuwa na ushindani mkubwa.
Ilikuwa ni Septemba 27 ambapo kazi ilianza kwa Mtibwa Sugar kusaka pointi tatu mbele ya Mbeya Kwanza ilikuwa Uwanja wa Mabatini, Kibaha na ngoma ilikamilika kwa ubao kusoma Mtibwa Sugar 0-1 Mbeya Kwanza.
Mtupiaji wa kwanza msimu wa 2021/22 ni nyota wa Mbeya Kwanza, Edgar William ambaye alifanya hivyo dakika ya 49 kwa shuti lake la mguu wa kushoto.
Katika mchezo mwingine wa pili ulikuwa ni ule uliowakutanisha Namungo na Geita Gold pale Lindi na ubao wa Ilulu ulisoma Namungo 2-0 Geita Gold.
Burudani nyingine tamu ilikuwa ni kati ya Coastal Union dhidi ya Azam FC pale Mkwakwani, Tanga na mwisho ubao ulisoma Coastal Union 1-1 Azam FC na kuwafanya wababe hao kugawana pointi mojamoja.
Kazi iliendelea kama kawaida ilikuwa ni Septemba 28 ambapo mchezo wa Dodoma Jiji dhidi ya Ruvu Shooting ulipigwa Uwanja wa Jamhuri, Dodoma.
Baada ya dakika 90, Cleophance Mkandala aliipa pointi tatu timu yake ya Dodoma Jiji baada ya kupachika bonge moja ya bao kwa shuti kali dakika ya 33 akiwa ametulia zake nje ya 18.
Pale Mbeya ilikuwa ni balaa ambapo bao la lala salama lilipachikwa na Peter Mapunda ambaye alikuwa akisoma mchezo nje na aliweza kupachika bao hilo dakika ya 90 na kufanya ubao wa Sokoine kusoma Mbeya City 1-0 Tanzania Prisons.
Bado burudani iliendelea ambapo ule mchezo uliokuwa na ushindani mkubwa ulikamilika kwa sare ya kibabe ambapo wote waliweza kugawana pointi mojamoja.
Ilikuwa Uwanja wa Karume ubao ulisoma Biashara United 0-0 Simba huku nahodha wa Simba, John Bocco akikutana na balaa la penalti yake ya dakika za lala salama kukwama mikononi mwa kipa wa Biashara United, James Ssetupa.
Baada ya Septemba 28 kufungwa kibabe huku Simba wakiwa ni mabingwa watetezi wakianza kwa mtindo wa kugawana pointi mojamoja ngoma iliendelea Septemba 29 kukamilisha mzunguko wa kwanza.
Mechi mbili zilichezwa ambapo ni Polisi Tanzania waliitungua KMC mabao mawili na mtupiaji akiwa ni Vitalisi Mayanga alifanya hivyo dakika ya 3 na dakika ya 20 huku nahodha Juma Kaseja akiwa hana chaguo pale Uwanja wa Karatu.
Mabingwa mara 27 wa Ligi Kuu Bara, Yanga wao kete yao ya kwanza waliifungulia huko Kagera baada ya ubao wa Uwanja wa Kaitaba kusoma Kagera Sugar 0-1 Yanga.
Bao pekee la ushindi lilifungwa na Feisal Salum dakika ya 24 kwa shuti lake la mguu wa kulia akiwa ndani ya 18 na kuipa pointi tatu muhimu timu yake kwenye mchezo huo ambapo alivaa kitambaa cha unahodha.
Mzunguko wa kwanza umekamilika na mechi nane zimechezwa huku jumla ya mabao 10 yakikusanywa ndani ya uwanja na kinara wa utupiaji ni Vitalis Mayanga wa Polisi Tanzania mwenye mabao mawili.
Pia kinara wa pasi za mwisho ni Obrey Chirwa wa Namungo mwenye pasi mbili na zote alitoa kwa mguu wa kulia.