Home news WAPYA KABISA LEO UWANJA WA MKAPA, SIMBA V YANGA

WAPYA KABISA LEO UWANJA WA MKAPA, SIMBA V YANGA


LEO Septemba 25 Uwanja wa Mkapa kunatarajiwa kuwa na mchezo wa kukata na shoka kati ya Simba v Yanga ambao ni wa Ngao ya Jamii.

 Mchezo huo ambao utakuwa ni wa ufunguzi wa msimu mpya wa Ligi Kuu Bara baada ya kumalizika kwa kipindi cha usajili na maandalizi ya msimu mpya unaotarajia kuanza Septemba 27.

Rekodi inaonyesha kwa mwaka huu Yanga na Simba hadi kufikia kwenye mchezo huo zitakuwa zimekutana mara tano katika mashindano yote.

Lakini katika mchezo huo wa Ngao ya Jamii umeanza kuzungumzwa kwa muda na mashabiki wa timu hizo kutokana na uwepo wa wachezaji wengi wapya ambao watakuwa wageni kwenye mchezo huo kwani ni mara yao kwanza kucheza mchezo wa dabi ambao ni mkubwa kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati.


Hapa tunakuletea wachezaji ambao watacheza kwa mara ya kwanza dabi hii kutoka kwenye vikosi vyote.


DJIGUI DIARRA- YANGA


Mrithi wa Metacha Mnata na Farouk Shikhalo ni kipa namba moja wa sasa wa Yanga kutoka nchini Mali, Djuigui Diara.

Kipa huyo ambaye licha ya kuonekana kuwa bora katika michezo aliyocheza lakini ameruhusu mabao manne katika mechi tatu, moja ikiwa ya kirafiki iliyoisha kwa Yanga kufungwa 2-1 na mbili za mashindano walizofungwa 1-0 kila moja.

YANNICK BANGALA- YANGA

Kiungo Mcongo mwenye uwezo wa kucheza nafasi ya beki wa kati na kiungo mkabaji, huyu ni kati ya wachezaji watakaokuwa wageni kwenye mchezo huo baada ya kujiunga na timu hiyo.

PETER BANDA-SIMBA

Unakumbuka Luis Jose Miquissone basi Peter Banda kutoka Malawi ndiyo amechukua mikoba yake hadi jezi yake lakini bado ni mchezaji mgeni kwenye mechi ya watani wa jadi.

Banda mwenye uwezo wa kucheza nafasi ya kiungo mshambuliaji anatajwa kuwa mmoja kati ya wachezaji wenye uwezo wa juu kwenye kikosi cha Simba hivyo atakutana na presha ya Simba na Yanga kwa mara ya kwanza leo Jumamosi.

FISTON MAYELE-YANGA

Kinara wa mabao wa AS Vita akiwa ingizo jipya ndani ya Yanga atakuwa ni mmoja wachezaji wakubwa wanaosubiriwa kwenye mchezo huo ambao kwake utakuwa wa kwanza dhidi ya Simba.

SOMA NA HII  SIMBA, YANGA VICHEKO TU KABLA YA KARIAKOO DABI

KHALID AUCHO- YANGA

Aucho hana ugeni sana na klabu za Tanzania kwa kuwa alishakutana nazo wakati anacheza Gor Mahia ya Kenya lakini atakuwa mgeni wa mchezo wa watani wa jadi ikiwa ni mara yake ya kwanza kucheza dhidi ya Simba akiwa Yanga.

SADIO KANOUTE – SIMBA

Sadio Kanoute mmoja kati ya viungo walioonyesha ukubwa wao katika mchezo wa Simba Day dhidi ya TP Mazembe kiasi cha mashabiki kupagawa. Kiungo huyo kutoka Mali ni ingizo jipya kwenye kikosi cha Simba na ni mgeni wa mechi ya watani.

DJUMA SHABANI -YANGA

Beki wa pembeni, Djuma Shabani yeye siyo mgeni na Simba lakini atakuwa ni mgeni kwenye mchezo huo akiwa Yanga kwa kuwa hajawahi kucheza mchezo huo.

ENOCK INONGA BAKA-SIMBA

Beki katili kutoka DR Congo, jamaa mmoja amepanda hewani, Enock Inonga Baka ni ingizo jipya ndani ya kikosi cha Simba na atakuwa mgeni wa mchezo wa dabi kwa kuwa utakuwa ni wa kwanza kwake.

 PAPE SAKHO- SIMBA

Pape Sakho ni kiungo mshambuliaji mpya ndani ya Simba lakini tayari ameshejenga utawala wake kutokana na kupendwa na mashabiki wengi wakiamini uwezo wake.

Kiungo huyo raia wa Senegal atakuwa ni miongoni mwa wachezaji wapya wa Simba na wageni wa mechi watani wajadi.


JESUS MOLOKO- YANGA

Winga teleza anayetajwa kuwa mrithi wa Tuisila Kisinda, Jesus Moloko kutoka DR Congo ni miongoni mwa wachezaji wapya wa Yanga na mgeni wa mchezo huo wa aina yake.

Wachezaji wengine ambao watakuwa wageni kwenye mchezo huo kwa upande wa Simba ni Duncan Nyoni, Abdul Swamad Kassim, Jimmyson Mwinuke, Jeremiah Kisubi, Denis Kibu na Israel Mwenda wakati Yanga ni Erick Johora, Dickson Ambundo, David Bryson na Yusuph Athuman.