Home news YANGA WAENDELEA KUZIFUNGA TIMU ZA DARAJA LA KWANZA..WAIKANDAMIZA DTB ‘TATU MZUKA’….

YANGA WAENDELEA KUZIFUNGA TIMU ZA DARAJA LA KWANZA..WAIKANDAMIZA DTB ‘TATU MZUKA’….


Yanga imecheza mechi nyingine ya kirafiki ya kujipima nguvu wakifanikiwa kushinda kwa mabao 3-1 dhidi ya DTB inayoshiriki Ligi Daraja la kwanza ‘Championiship’.

Katika mchezo huo uliopigwa jioni ya leo katika Uwanja wao wa mazoezi katika kambi yao ya Avic iliyopo Kigamboni nje kidogo ya jijini Dar es Salaam, Yanga ndio waliokuwa wa kwanza kupata bao likifungwa na mshambuliaji Fiston Mayele akimalizia pasi ya Dickson Ambundo.

Hata hivyo bao hilo halikudumu DTB wakisawazisha kupitia Said Chunga na kufanya timu zote kwenda mapumziko matokeo yakiwa sare ya bao 1-1.

Kipindi cha pili Yanga walirudi na nguvu na kufanikiwa kupata bao la pili likifungwa na beki wao mpya David Bryson kwa shuti kali la umbali mrefu.

Yanga ikiwatumia wachezaji ambao walikosa nafasi ya kucheza mechi mbili za Ligi ya Mabingwa Afrika na wale waliocheza kwa muda mchache walifanikiwa kupata bao la tatu likifungwa na mshambuliaji Yusuf Athuman.

Athuman alifunga bao hilo akifanikiwa kuinasa pasi fupi ya beki wa DTB Yusuf Mlipili kisha mfungaji kumpiga chenga kipa na kufunga kirahisi.

Mapema kocha Nesreddine Nabi mara baada ya kikosi chake kuondolewa katika Ligi ya Mabingwa alitaka mchezo huo  ili apate nafasi ya kuwarudishia ubora wachezaji wake ambao hawakupata muda wa kucheza.

Akili hiyo ya Nabi inalenga kutanua wigo wa kuchagua wachezaji wake kuelekea maandalizi ya kuvaana na watani wao Simba katika mchezo wa Ngao ya Hisani utakaopigwa wikiendi hii Septemba 25 kwenye Uwanja wa Mkapa.

SOMA NA HII  BAADA YA KUICHEULIA TFF KUWA KOCHA WA STARS....NABI AFUNGUKA HAYA KUHUSU KOCHA MPYA...