JWANENG Galaxy ya Botswana, imepanga pambano lao la kwanza dhidi ya Simba lipigwe saa 9:00 alasiri sawa na saa 10:00 jioni za Tanzania.
Kwa mujibu wa rekodi za Mamlaka ya Hali ya Hewa ya Botswana, muda huo wa saa 9 hali ya hewa ya nchini humo itakuwa nyuzi joto 29 mpaka 30 ambalo ni sawa na lile la Dar es Salaam ambako Simba hucheza saa 10. Ikiwa ni pungufu na iliyokuwa jana na leo ambayo ipo kati ya nyuzijoto 36-37.
Hata hivyo, mabosi wa Msimbazi wamesisitiza kwamba wamejipanga ndani na nje ya uwanja na kila kitu kitakwenda sawa.
Akizungumza Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya klabu hiyo, Mulamu Nghambi alisema kikosi chao kitaondoka leo Ijumaa jioni na ndege ya kukodi moja kwa moja hadi Botswana na kurudi. Msafara wa timu hiyo unaenda wakipishana saa chache tu na vigogo wawili wa klabu hiyo wameondoka jana kwenda kuungana na mratibu wao, Ally Abbas na Mpishi Samwel ‘Sam’ Mtundu waliotangulia mapema wiki hii.
Mulamu alifafanua pia ishu yao na Shirika la Ndege, ATCL na kusema waliingia mkataba kusafiri na shirika hilo ndani na nje ya nchi, ila kwa bahati mbaya hawana ruti ya safari Botswana hivyo imewafanya wakodi ndege nyingine itakayowapeleka na kuwarudisha kutoka huko.
“Kuhusu mchezo wetu wa Ligi, tuliomba usogezwe kwani ni ngumu kucheza tarehe iliyopangwa kwa mabadiliko ya CAF juu ya mchezo wetu uliopangwa awali upigwe Oktoba 15 hna kupelekwa hadi 17 hivyo hatukuwa na jinsi ndio maana tuliomba mchezo wetu na Polisi Tanzania nao usogezwe.
“Mchezo huo tulitakiwa upigwe Oktoba 20, nasi tunarudi Jumatatu baada ya mechi, hiyo kisha tucheze siku moja baadaye halafu Oktoba 24 turudiane na Galaxy ni kitu kisichowezekana kiuhalisia, ndio maana tumefanya hivyo,” alisema Mulamu mmoja ya watu wenye ushawishi mkubwa Simba.
Naye Mratibu Ally Abbas aliliambia gazeti la Mwanaspoti kwa njia ya simu kutoka Botswana, maandalizi kwa upande wao yako vizuri na wanasubiri siku ya mchezo na imani yao ni ushindi tu.
“Huku kila mtu yuko bize na mambo yake, kila mtu anapambana na Uviko 19 hata habari za mpira hawana kabisa, huko Tanzania ndio mnajua Simba aitacheza, lakini huku hawana habari kila mtu yuko bize na ishu zao,” alisema na kuongeza hakuna mzuka mitaani kama mataifa mengine waliyowahi kwenda kwa mechi hizo za Afrika.