KIKOSI cha Simba jioni ya leo kipo uwanjani kupeperusha bendera ya taifa kimataifa kwa mara ya kwanza msimu huu kuvaana na Jwaneng Galaxy, ikiwa bila kiungo wake na mchezaji mwandamizi, Jonas Mkude aliyeachwa kwenye msafara wa wachezaji 24 walioenda Botswana.
Simba ipo Gaborone na wachezaji 24, bila ya Mkude wala Chris Mugalu ambaye ni majeruhi pamoja na nyota wake wapya iliyowasajili msimu huu, Pape Ousmane Sakho, kipa Jeremia Kisubi na straika Denis Kibu wenye matatizo tofauti ikiwamo majeruhi na kutokuwepo kwenye usajili wa Caf.
Hata hivyo, Mkude si majeruhi, bali aliachwa kutokana na kushindwa kuendana na falsafa ya Kocha Didier Gomes aliyesisitiza mazoezini viungo kuwa watulivu wanapokuwa na mpira na kuhakikisha wanapiga pasi fupifupi za uhakika na sio ndefu zinazopotea.
Katika mazoezi yaliyokuwa yanafanyika Uwanja wa Boko Veterani, Gomes alionekana akiwaelekeza mara kwa mara wachezaji hao jambo ambalo Mkude alishindwa kuendana nalo, hivyo kuenguliwa kwenye timu iliyosafiri.
Akizungumzia mchezo huo beki wa kulia wa timu hiyo Israel Patrick Mwenda, alisema utakuwa mgumu ila wamejipanga kuhakikisha wanaibuka na ushindi.
Naye kocha msaidizi wa zamani wa Gwambina FC, Athuman Bilali alisema licha ya Simba kuanza kwa kusuasua Ligi Kuu, anaiona ikiendelea kufanya vizuri kwenye michuano ya kimataifa.