KOCHA mkuu wa Simba, Didier Gomes ametamba kuwa ana matarajio makubwa ya kikosi chake kufikia malengo yao ya kucheza hatua ya nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu.
Simba juzi Jumapili ilianza kibarua chake cha kwanza kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu, ambapo walikuwa ugenini nchini Botswana wakicheza dhidi ya Jwaneng Galaxy, mchezo uliopigwa kwenye Uwanja wa Taifa wa Botswana na kufanikiwa kuibuka na ushindi wa goli mbili bila.
Baada ya mchezo wa juzi, Simba sasa wanatarajia kurudiana na Galaxy Jumapili ya Oktoba 24, mwaka huu kwenye Uwanja wa Mkapa Dar es Salaam. Katika michuano hiyo msimu uliopita, Simba waliondolewa katika hatua ya robo fainali baada ya kufungwa jumla ya mabao 4-3 na Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini.
Gomes alisema: “Msimu uliopita tuliwathibitishia watu kuwa Simba ni miongoni mwa timu nane bora zaidi ndani ya Afrika kwa sasa na ndiyo maana tulichaguliwa kuwa miongoni mwa timu kumi ambazo hazikucheza hatua ya awali ya michuano ya mwaka huu, hivyo ni wazi tuna kazi kubwa ya kuendelea pale tulipoishia.
“Msimu huu mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika ndiyo kipaumbele chetu namba moja, na tumejiwekea malengo ya kuhakikisha tunafika hatua ya nusu fainali, kwa namna ninavyokiona kikosi changu sina shaka na hilo naamini tuna wachezaji bora na wenye uzoefu wa kutufikisha hapo.”