Home news GOMES AWAWEKA CHONJO SAKHO, NYONI NA BANDA…ASEMA BADO HAWAFITI KUCHEZA SIMBA..

GOMES AWAWEKA CHONJO SAKHO, NYONI NA BANDA…ASEMA BADO HAWAFITI KUCHEZA SIMBA..

 


KOCHA Mkuu wa Simba, Didier Gomes amesema wachezaji wake wapya Pape Sakho, Duncan Nyoni na Peter Banda wanahitaji muda zaidi kuingia moja kwa moja kwenye kikosi chake.

Sakho, Nyoni na Banda waliosajiliwa msimu huu hawaingia moja kwa moja katika kikosi cha Simba.

Gomes alisema wachezaji hao ni wazuri na ndio maana walisajiliwa, lakini kucheza wanahitaji muda.

“Kikosi changu kina wachezaji wengi wapya msimu huu. Wanahitaji muda wa kuzoeana na wenzao na kufanya vizuri, lakini hadi sasa wanazidi kuwa bora kadri siku zinavyokwenda,” alisema Gomes.

“Sadio Kanoute, Sakho na Nyoni wanakuja vizuri na naamini watakuja kuleta vitu vizuri siku za mbele. Najiamini sana kutakuwa na mambo mazuri siku za mbele, wachezaji wote wanabadilika kiuchezaji.”

Gomes alisema kuondoka kwa Clatous Chama na Luis Miquissone kunamtaka atengeneze aina nyingine ya washambuliaji ili timu iendelee kufanya vizuri.

“Tumeanza kubadilika eneo la ushambuliaji. Kiukweli kuondoka kwa Luis na Chama unatakiwa utafute njia nyingine ya kwenye ushambuliaji. Tupo njia sahihi mpaka sasa,” alisema.

Sakho kwenye mechi za mashindano alianza na Ngao ya Jamii dhidi ya Yanga na mechi ya Dodoma Jiji ya Ligi Kuu Bara tu katika mechi tatu ambazo Simba wamecheza, huku Banda aliingia dhidi ya Yanga (Ngao ya Jamii) na mechi ya Biashara na Dodoma Jiji.Naye Nyoni aliingia akitokea benchi katika Ngao ya Jamii, Biashara na Dodoma Jiji.

Hata hivyo kina Banda na Nyoni licha ya kutoanza kikosi cha kwanza wamekuwa wakiitwa timu ya taifa ya Malawi ambayo imecheza mechi za kuwania kufuzu Kombe la Dunia, Qatar 2022.

SOMA NA HII  KLABU YA PATRICK AUSSEMS MAJANGA MATUPU, FIFA KUIPIGA PINI USAJILI