HIZI mechi tano zijazo, kuna mtu atalia. Yaani kama Yanga itachanga vyema karata zake katika mechi hizo 5 za Ligi Kuu Bara, itawavuruga ile mbaya wapinzani wake Simba na Azam FC kwa kuweka pengo kubwa la pointi na kujitengenezea mazingira rafiki ya kutwaa ubingwa msimu huu.
Mechi hizo ndizo tano zinaonekana kikwazo kikubwa kwa Yanga katika mzunguko wa kwanza zikihusisha wababe wote wa mbio za ubingwa kwani baada ya hapo watakuwa na mechi sita dhidi ya timu ambazo hazionekani kama tishio kubwa kwao.
Hiki ni kibarua kizito cha kufungia mwaka kwa mastaa wa Yanga kina Fiston Mayele, Fei Toto na wenzao ambacho kinatamatika Desemba 11 kwa mechi ya kibabe dhidi ya mahasimu wao wa jadi, Simba.
Kibarua cha Yanga kitaanza kwa mchezo dhidi ya Azam FC utakaochezwa Jumamosi, Saa 1.00 usiku kwenye Uwanja wa Mkapa na kama Yanga itaibuka na ushindi, itaipiku Azam kwa pointi nane kwani hadi sasa wako mbele yao pointi tano.
Baada ya hapo, Yanga itaikaribisha Ruvu Shooting kwenye uwanja huo huo wa Mkapa, Oktoba 2, kuanzisha saa 12.15 jioni na ikitoka hapo itasubiri hadi Oktoba 20 itakaposafiri hadi Lindi kuvaana na Namungo FC.
Ikumbukwe Namungo FC ni miongoni mwa timu ambazo misimu miwili iliyopita imechangia kuipunguza kasi Yanga katika mbio za ubingwa kwani mechi zote walizokutana za ligi, walitoka sare hivyo kama Yanga watapata ushindi ugenini itakuwa ni karata muhimu katika mbio za ubingwa.
Yanga ikimalizana na Namungo FC, mchezo utakaofuata itaenda hadi Mbeya kukabiliana na wabishi wa Mbeya Kwanza, Novemba 30 kwenye Uwanja wa Sokoine mkoani humo.
Na baada ya hapo, Yanga itarudi Kwa Mkapa, kuvaana na watani wao wa jadi, Simba, Desemba 11 ambao umepangwa kuanza saa 11.00 jioni.
Ikiwa Simba nao watapata ushindi katika mechi zote zilizo mbele yao kabla ya kuvaana na watani wao, maana yake Yanga ikiibuka na ushindi katika mchezo huo, itawapiku Simba kwa pointi tano zaidi na kujikita kileleni mwa msimamo wa ligi.
Mambo yanaweza kuwa mazuri zaidi kwa Yanga ikiwa Simba na Azam wataangusha pointi katika baadhi ya michezo kabla ya kukabiliana nao kwani itazidi kufanya pengo la pointi kati yao liwe kubwa zaidi.
Lakini kama Yanga watavurugwa katika mechi hizo tano, wapinzani wao Simba na Azam watakuwa na nafasi ya kuwapita kwa kasi kama ya roketi.
Azam baada ya kucheza na Yanga, Jumamosi hii, mechi zao nne ni za nyumbani dhidi ya Geita Gold, Kagera Sugar, Mtibwa Sugar na Mbeya City huku moja ya ugenini ikiwa dhidi ya KMC.
Kwa upande wa Simba, kabla ya kuvaana na Yanga, itakuwa na mechi tano na nne zitakuwa nyumbani dhidi ya Polisi Tanzania, Coastal Union, Geita Gold na Namungo wakati mechi moja itakuwa ugenini dhidi ya Ruvu Shooting.
Mjumbe wa kamati ya mashindano Yanga, Hersi Said alisema hawana lengo la kushinda mechi tano pekee bali wanachokiangalia sasa ni kushinda kila mchezo ulio mbele yao.
“Kila mechi iliyo mbele yetu tunaichukulia kama fainali, tunawaheshimu wapinzani wetu wote, hatuna timu changa wala kongwe kwenye ligi, tunaamini katika ushindani. Malengo yetu msimu huu ni kukusanya pointi kwenye kila mchezo hivyo maandalizi ya timu yanatakiwa kuzingatia kila eneo,” alisema na kuongeza;
“Kwa upande wetu viongozi tumefanya kila linalowezekana kuhakikisha tunasajili wachezaji wa maana ili kurudisha timu kwenye ushindani na sasa tunawaachia wachezaji wafanye kile wanachoelekezwa na kocha, lengo likiwa ni moja tu kukusanya pointi kwenye kila mchezo.”
Naye Mkurugenzi wa Mashindano wa Yanga, Thabit Kandoro, alisema wameshinda michezo mitatu hadi sasa hivyo kushinda mitano iliyo mbele yao haiwezi kuwapa picha ya ubingwa zaidi itawaweka kwenye ramani nzuri ya kufikia mafanikio.
“Tuna mechi tano ngumu mbele yetu na kila mchezo una thamani ya pointi tatu, tunatambua ugumu wa ligi msimu huu lakini mipango yetu ni kuhakikisha tunatwaa taji la ligi na hatutadharau mechi yoyote, zote tutazichukulia kwa uzito,” alisema na kuongeza;
“Sio rahisi kukusanya pointi hizo bila maandalizi, kocha ana kazi ya kufanya kuhakikisha anaandaa kikosi kwa upana ili kila mchezaji aweze kuwa kwenye ari nzuri ya kushindana na mbinu zote za kiufundi zitatumika.”