Baada ya kuachana na Simba SC, Kocha Didier Gomes amempa ushauri wa bure kiungo Jonas Mkude ambaye hajaonekana kikosini kwa muda mrefu.
Gomes alivunja mkataba na Simba SC kama sehemu ya kukubali kuwajibika na matokeo ya mabao 3-0, yaliyoifika klabu hiyo dhidi ya Jwaneng Galaxy ya Botswana Jumapili (Oktoba 24).
Kocha huyo kutoka nchini Ufaransa amesema Mkude anapaswa kubadilisha mwenendo wa maisha yake ya soka ili aweze kurudi kwenye kikosi cha kwanza cha Simba SC.
“Mkude namuamini na naamini katika uwezo wake na kipaji, lakini ili uweze kufikia malengo unatakiwa kutumia muda mwingi kufanya mazoezi utafika mbali zaidi ya hapa ulipo sasa, kama amenielewa na kukubaliana na kauli yangu nina imani atakuwa bora na ataisaidia Simba,” anasema Gomes na kuongeza;
“Suala la kucheza kwenye kikosi cha Simba bado lipo kwenye mikono yake yeye mwenyewe Mkude.Lwanga (Tadeo), Sadio (Kanoute), Mzamiru (Yassin) na Erasto (Nyoni) wote ni wazuri kwenye kiungo lakini kila moja ana staili yake ya kucheza.”
“Kila mchezaji nimewahi kumpa nafasi ya kucheza hii inaonyesha nilikuwa naelewa umuhimu wao kikosini, shida ni kwa Mkude ambaye sijamtumia mara nyingi hivi karibuni kwasababu hajafanya mazoezi na timu muda mrefu,” anasema na kuongeza:
“Hakuna mchezaji ambaye hakuwa na namba kwenye kikosi changu, ukiona mchezaji sijamtumia basi kashindwa kunishawishi mazoezini na amekosa moja ya programu zangu kuelekea mchezo husika.”