Home Makala LIGI KUU BARA IMEANZA, MAKOSA YAFANYIWE KAZI

LIGI KUU BARA IMEANZA, MAKOSA YAFANYIWE KAZI


 AKILI za wengi kwa sasa zimeelekezwa kwenye mwanzo wa Ligi Kuu Bara ambayo imeanza kwa spidi inayopendeza na kufurahisha pia.


Hili ni jambo jema kwa sababu tumeona mwanzo wa ligi tu kuna mambo yanayovurugavuruga mipango yameanza kujitokeza haya yanapaswa yatazamwe kwa umakini mkubwa ili kuifanya ligi kuwa imara na ushindani mkubwa.


Hiana maana kwamba haya mambo ambayo yanatokea yanawezwa kumalizwa kabisa haiwezekani ila kinachowezekana ni kupunguza ama kuboreshwa kwa ajili ya wakati ujao.

KMC inakumbuka namna ratiba yake ilivyozunguka kwa upande wa uwanja kwenye mchezo wao dhidi ya Polisi Tanzania ambao ulichezwa Uwanja wa Karatu ambapo kuna jambo liliwavuruga mashabiki pamoja na timu husika.

Ishu kubwa ilikuwa ni kwenye uwanja ambapo awali ulipangwa kutumika ule Uwanja wa Ushirika Moshi ila mwisho wa siku wakabadili na kuupeleka Uwanja wa Sheikh Amri Abeid.

Ngoma kabla haijachezwa unaambiwa mchezo ukabadilishwa na kupelekwa Karatu, kazi inaanza mapema kabisa ambapo timu zimeanza kuvurugika mapema sawa na mashabiki pia.


Timu zote mbili zilivurugwa kwenye mchezo huo ila mwisho wa siku mchezo ulichezwa na mshindi akawa ni Polisi Tanzania ambaye alishinda kwa mabao 2-0.


Hakuna namna ya kuzuia makosa yatokee ila kuna namna ya kuweza kuyaboresha na kuyafanya yasirudie tena wakati mwingine.


Jambo la msingi ni mamlaka kuwa na mpango kazi mzuri kwenye suala la upangaji wa ratiba pamoja na ishu ya matumizi ya sehemu ya kuchezea.


Ipo wazi kwamba suala la uwanja ni tatizo kwa timu nyingi Bongo kwani hata Mtibwa Sugar wenyewe hawapo pale Jamhuri Morogoro na badala yake kwa sasa wapo zao Kibaha wakitumia Uwanja wa Mlandizi.


Hapa ni pakuanzia kuanzia mamlaka zinazosimamia viwanja pamoja na timu kuweza kujipanga vema kwa ajili ya msimu mpya ili waweze kupata matokeo mazuri katika uwanja ambao waliuzoea.


Ikumbukwe kwamba kesi ya kubadili uwanja kwa Mtibwa Sugar iliwagharimu msimu uliopita ambapo awali walikuwa wanatumia ule Uwanja wa Manungu kisha baadaye ikawa Gairo kabla ya kuhamia Uwanja wa Jamhuri, Morogoro.

SOMA NA HII  MORRISON AFUATA NYAYO ZA OKWI SIMBA NA YANGA....ACHOTA MAMILIONI YA PESA PANDE ZOTE KIULAINII...


Ukweli ni kwamba gharama ambazo wanazitumia kwa sasa Mtibwa Sugar kufika hapo ambapo inapaswa wacheze ni kubwa tofauti na zile ambazo wangezitumia pale Uwanja wa Jamhuri.


Yote haya yalipaswa yapangwe mapema ikiwa ni suala la maandalizi ni muhimu kuweza kujipanga mapema ili kila mmoja aweze kwenda sawa na kasi ya matumizi ya mkwanja pia. 

Pia ni wakati sahihi kwa wale wenye timu kuweza kupanga mkakati wa kuweza kuwa na viwanja vyao wenyewe hii itaondoa haya matatizo yanayotokea mara kwa mara.

Pia kwa vle ambavyo vipo ni muhimu kuweza kuviboresha ili viwe safi kwa ajili ya matumizi ya mechi za ushindani.