Home Makala WAMEANZA NA MAJANGA MSIMU MPYA WA 2021/22, SIMBA WANAWEZA KUKOSA UBINGWA

WAMEANZA NA MAJANGA MSIMU MPYA WA 2021/22, SIMBA WANAWEZA KUKOSA UBINGWA

 


 IKIWA Simba watakuwa kwenye mwendo huu ndani ya msimu wa 2021/22 kengele ya hatari inawaka kwenye kichwa cha Kocha Mkuu, Didier Gomes kwa kuwa kutakuwa na hatihati ya kuachia ubingwa kwa wapinzani wao pamoja na kushindwa kufurukuta kwenye mechi za kimataifa.


Hili linakuja kutokana na rekodi kuonyesha kwamba wachezaji wake wengi muhimu wamekuwa wakikutana na minyoosho ya maana huku Gomes akikiri kwamba ligi ni ngumu na ushindani ni mkubwa.


Iliwatokea Liverpool ya Ulaya msimu uliopita baada ya kuwakosa nyota wake muhimu kutokana na kupatwa minyoosho uwanjani miongoni mwao alikuwa ni beki kisiki Virgil van Djik ambaye aligongwa na alikaa nje msimu mzima wa 2020/21 na timu yake ikapoteza ubingwa.


Hapa Championi Jumatatu inakuletea orodha ya wachezaji walioanza na majanga 2021/22 huku Simba ikiwa ni namba moja kwa timu yenye wachezaji wengi wenye majanga:-


Joash Onyango

Beki kisiki wa Simba hana bahati na mechi kubwa kwa kuwa aliwahi kupata maumivu kwenye mchezo dhidi ya Kaizer Chiefs na kumfanya akae nje kwa muda.

Msimu huu wa 2021/22 Septemba 25 inaishi kichwani mwake kwa kuwa alikwama kukamilisha dakika 90 baada ya kuumia kichwa. Amekosa mechi mbili ilikuwa dhidi ya Biashara United na Dodoma Jiji.


Kapombe

Shomari Kapombe, maumivu ya enka aliyopata kwenye mchezo dhidi ya Biashara United yalimfanya aanze kwa majanga na alikwama kukamilisha dakika zote 90 nafasi yake ilichukuliwa na Mohamed Hussein, ‘Tshabalala’.

Kanoute

Sadio Kanoute, alipata maumivu kwenye mchezo wa Ngao ya Jamii, Septemba 25 dhidi ya Yanga ingizo hili jipya linapewa nafasi ya kufanya vizuri kutokana na uwezo wake.Mechi ya Biashara United na ile ya Dodoma Jiji zote kazikosa.


Kennedy

Kennedy Juma alipata maumivu ya kichwa baada ya kuonekana akipigwa kiwiko na mchezaji wa Dodoma Jiji, Anuary Jabir. Ilikuwa ni mchezo wake wa pili kucheza ndani ya ligi baada ya kuanza ule dhidi ya Biashara United na wa pili aliumia mbele ya Dodoma Jiji.

Lwanga

Mkata umeme alianza kwa majanga msimu wa 2021/22 baada ya kuonyeshwa kadi mbili za njano Septemba 25 kutokana na kucheza faulo kwa Feisal Salum jambo lililofanya aonyeshwe kadi nyekundu.

Alikosa mchezo dhidi ya Biashara United ila Lwanga anamerejea kwenye mchezo dhidi ya Dodoma Jiji naye alipata maumivu ya mguu baada ya kuchezewa faulo kwenye mchezo  huo.

SOMA NA HII  SURA YA KAZI, KIUMBE ANAYETAJWA KUTWAA MATAJI MENGI


Sakho

Pape Sakho alipata maumivu ya mguu baada ya kugongwa kwenye mchezo wa ligi dhidi ya Dodoma Jiji.Ilikuwa ni mchezo wake wa pili kwenye ligi alicheza ule wa Biashara United na wa pili ulikuwa dhidi ya Dodoma Jiji mwisho alipata majanga.

Bocco

John Bocco, nahodha wa Simba alianza msimu wa 2021/22 kwa majanga baada ya  kukosa penalti kwenye mchezo wa ligi dhidi ya Biashara United ya Mara baada ya kipa James Ssetupa kuokoa mchomo huo.


Jambo hilo lilifanya Simba kugawana pointi mojamoja na Biashara United.


Azam FC

Hawa kinara wao wa utupiaji kwa msimu wa 2020/21 ambapo alitupia mabao 14 na pasi tano Prince Dube yupo nje kutokana na tatizo la kushindwa kukunjuka kwa msuli wa tumbo upande wa kushoto na alifanyiwa upasuaji Afrika Kusini.

Kwa sasa tayari mapumziko aliyopewa muda wake umeisha kwa mujibu wa Ofisa Habari wa Azam FC, Zakaria Thabit ameanza kufanya mazoezi.Alikosekana kwenye mchezo dhidi ya Coastal Union ambao ulikuwa ni wa ufunguzi.

Morris

Nahodha huyu Aggrey Morris amesimamishwa na mabosi wake ilikuwa ni Oktoba 6,2021 kwa muda usiojulikana.

Sure Boy

Salum Abubakary, ‘Sure Boy’ nahodha huyu msaidizi wa Azam FC naye alisimamishwa Oktoba 6,2021.

Mudhathir

Mudhathir Yahya naye alisimamishwa Oktoba 6,2021 kwa kile ambacho kilielezwa kuwa sababu ya nyota hao watatu kusimamishwa ni utovu wa nidhamu kwa meneja wa timu, Luckson Kakolaki, Septemba 18,2021.


Dodoma Jiji


Anuary Jabir wa Dodoma Jiji anakuwa ni mchezaji wa kwanza kwa msimu wa 2021/22 kuonyeshwa kadi nyekundu ya moja kwa moja alipomchezea faulo Kennedy Juma wa Simba.


Joseph Akamba alikuwa mwamuzi wa mchezo huo uliochezwa Uwanja wa Jamhuri,Dodoma.


Yanga



Mapinduzi Balama huyu ameshapona lakini hakuwa uwanjani kwa muda mrefu na msimu wa 2020/21 hakucheza mchezo hata mmoja kutokana na kusumbuliwa na maumivu ya enka.

Yassa

Yassin Mustapha ambaye ni beki naye aliumia msimu uliopita huku Bakari Mwamnyeto ambaye ni nahodha alikosa mchezo dhidi ya Kagera Sugar na ule dhidi ya Geita Gold kutokana na kusumbuliwa na maumivu.


Muhimu


Matukio ya wachezaji kugongana uwanjani huwezi kukwepa lakini ni muhimu kila mchezaji kuwa mlinzi wa mchezaji mwingine, afya kwanza.