Home news GOMES AMUAMULIA MKUDE…AMBADILISHA NAMBA..SASA KUCHEZA PACHA NA ‘VARANE’

GOMES AMUAMULIA MKUDE…AMBADILISHA NAMBA..SASA KUCHEZA PACHA NA ‘VARANE’


MASHABIKI wa Simba waliokuwa kwenye mazoezi ya juzi jioni waliona kitu cha ajabu kidogo. Kocha Didier Gomes, alimchezesha kiungo Jonas Mkude kwenye nafasi ya beki Joash Onyango.

Onyango alikuwa kwenye timu yake ya Taifa ya Kenya ambako alichezeshwa dakika 45 tu kama beki wa kulia wakilala mabao 5-0.

Katika kuonyesha kuwa amepania na anataka wachezaji wake kucheza nafasi tofauti uwanjani juzi jioni kocha Gomes alimpanga Mkude kucheza beki wa kati sambamba na Enock Inonga’Varane’, nafasi ambayo aliicheza kwa ufanisi mkubwa na kuwashangaza wengi ambao muda wote walikuwa wakimjadili.

Gomes alipanga vikosi viwili – kimoja kiliongozwa na kipa Beno Kakolanya, Mkude, Inonga, Ibrahim Ajib, Dennis Kibu, Yusuph Mhilu, Abulswamad Kassim na wachezaji watatu wa timu ya vijana wakati kingine kilikuwa na kipa Jeremia Kisubi, Kennedy Juma, Pascal Wawa, Shomari Kapombe, Gadiel Michael, Hassan Dilunga, Erasto Nyoni, John Bocco, Mzamiru Yassin, Benard Morrison na Sadio Kanoute.

Mkude alicheza kwa umahiri akishirikiana na Inonga kuokoa hatari zilizoelekezwa golini kwao na kufanya mashabiki kumpigia makofi mara kwa mara huku wakishangazwa na kiwango alichokionyesha.

Kocha mzoefu, Mrage Kabange alisema Gomes amefanya vizuri kumbadili nafasi Mkude kwani anaweza kusaidia pindi mabeki watakapokuwa majeruhi.

“Ujue kwenye mpira kuna mambo mengi, kuna siku inaweza bahati mbaya ikatokea mabeki wa kati wana kadi au wameumia sasa kocha ukishaanza mapema kuwaandaa wengine kucheza nafasi tofauti uwanjani inakupa urahisi wa kutopata presha kwani yoyote anaweza akacheza kwa ufanisi, “alisema Kabange.

Wachezaji ambao hawakuhudhuria mazoezi ni Mugalu na Sakho ambao ni majeruhi wakati Peter Banda, Duncan Nyoni (Malawi), Joash Onyango (Kenya) na Meddie Kagere (Rwanda) walikuwa hawajarejea kutoka katika majukumu ya timu zao za Taifa lakini jana jioni walitarajiwa kuwepo.

Gazeti la Mwanaspoti lilishuhudia vita mpya kwenye kila nafasi kuanzia eneo la kipa mpaka ushambuliaji. Muda mwingine Mkude na Benard Morisson walikuwa wakitumia zaidi nguvu na kuwania mipira huku kila mmoja akitaka kumuonyesha kocha kitu na akavutiwa kwani alitaka kuona kila mchezaji anapambana.

SOMA NA HII  MWAMUZI AFUNGUKA UTATA WA PENATI ZILIZOOKOLEWA NA ALLY SALIM DHIDI YA YANGA JUZI...

Gomes alisema hakuna mchezaji mwenye nafasi ya uhakika kucheza, bali atazingatia kile kinachoonyeshwa mazoezini kwa kuzingatia anachofundisha na mazingira ya mechi husika.