Home BIashara United ADAM SALAMBA: – NALIPWA MILIONI 161..AFUNGUKA JINSI ALIVYOJIUNGA NA TIMU YA MATAJIRI...

ADAM SALAMBA: – NALIPWA MILIONI 161..AFUNGUKA JINSI ALIVYOJIUNGA NA TIMU YA MATAJIRI WA ALGERIA..ATAJA MADEM…

 


BAADA ya kusaini mkataba wa miaka mitatu na JS Saoura ya Algeria, straika Mtanzania Adam Salamba anafunguka safari yake ilivyokuwa hadi kufanikisha dili hilo lililompa mkwanja mrefu unaomfanya aishi kifahari.

Nyuma ya mafanikio hayo, Salamba anakumbuka akiwa mdogo, aliweka dhamira ya soka kumfuta machozi na kumfanya aishi vizuri.

“Wazazi wangu walifariki nikiwa mdogo, nilianza kucheza mechi za mtaani nikiwa na miaka 10, ambapo chochote nilichokuwa nikipewa nilikuwa nampelekea mama yangu mdogo ambaye ni pacha wa mama.

“Ugumu wa maisha ulinifanya niweke dhamira kwa Mungu kwamba nikikua nahitaji soka linipatie pesa, nikaanza safari yangu Stand United, Lipuli ya Iringa, kisha nikaanza kuona matunda Simba ambayo ilinifungulia njia hadi sasa,” anasema Salamba.

SAFARI YA KUTUA JS SAOURA

Salamba anasema mwenyekiti wa klabu ya JS Saoura, alikuwa anamfuatilia tangu alipokuwa anaichezea Al Jahra ya Kuwait na kama isingekuwa ishu ya Uviko 19 kuingilia kati asingerejea Tanzania mwaka 2019.

“Wakati nacheza Kuwait huyo mwenyekiti aliwahi kunifuata kutaka nikaichezee timu yao, lakini kipindi hicho ugonjwa wa Uviko19 ulipamba moto na ndio sababu ya kuvunja mkataba na Al Jahra,” anasema.

Anasema wakati yupo Namungo, kiongozi huyo alimtafuta tena ili akafanye naye kazi lakini dirisha la usajili la Algeria lilikuwa limefungwa.

“Baada ya msimu uliopita wa ligi kumalizika wakanitafuta tena ndipo nikamwambia wakala wangu aongee nao. Wakaniambia niende kufanya majaribio ya wiki mbili, nikafanya na kufaulu kisha nikasaini mkataba wa miaka mitatu,” anasema.

Salamba anatoa elimu kwa mastaa wengine, waliopata changamoto nje, kisha wakarejea nyumbani kuwa wasikate tamaa kuendelea kutafuta konekisheni za timu kutoka nchi mbalimbali.

“Wakati nacheza Kuwait na kiongozi wa JS Saoura kunifuatilia na kupenda uchezaji wangu na urefu nilionao, nilitengeneza koneksheni na watu wengine kutoka timu mbalimbali niliokuwa nawasiliana nao mara kwa mara kubadilishana mawazo ya kazi,” anasema.

PESA ANAYOPATA KWA MWAKA

Baada ya Salamba kuvuta mkwanja mrefu wakati anacheza Al Jahra ya Kuwait, kwa sasa mchezaji huyo anapata fedha nyingi zaidi katika klabu ya JS Saoura.

Anasema kwa mwaka analipwa Sh161 milioni za Kitanzania, pia ndani ya mkataba wake wanaposhinda mechi mechi moja wanapata Euro 500 (takriban Sh1.3 milioni) na wakati mwingine hupata hadi Euro hadi 600 (takriban Sh1.6 milioni).

SOMA NA HII  JEMBE:MPIRA WA TANZANIA UNAPASWA KUPEWA THAMANI

“Nimejisikia faraja baada ya kupata kibali mbele ya viongozi na wachezaji wenzangu na tayari nimepata marafiki kibao hivyo sina upweke kama nilivyokuwa naishi Kuwait,” anasema.

VYAKULA CHANGAMOTO

Salamba anasema changamoto ya chakula ni kama ilivyokuwa wakati yupo Kuwait ambako chakula chao kilikuwa ni chapati, tambi, kuku na nyama, huku upatikanaji wa ugali na wali unakuwa mgumu.

“Tangu nifike huku sijawahi kukutana na ugali wala wali na mazingira ya huku yanaendana na Kuwait,” anasema mshambuliaji huyo ambaye hadi sasa amedumu nchini humo kwa wiki tatu.

Salamba anasema lugha pia ni changamoto nyingine kwake nchini humo. Anasema: “Wanazungumza Kifaransa na Kiarabu ambacho nakifahamu kwa sehemu, hivyo hainisumbui sana kuelewana na watu,” anasema.

Wakati yupo Kuwait, Salamba aliwahi kukaririwa na  Gazeti la Mwanaspoti kwamba, ilikuwa ngumu kuonana na mwanamke, maana ni nchi iliyotawaliwa sharia za dini ya Kiislamu.

Anazungumzia kwa upande wa Algeria kwamba bado anaendelea kusoma utamaduni wao, siku hadi siku ili kuweza kuendana nao.

“Kwa sasa nakaa kwenye hoteli ya nyota tano wakati nasubiria mchakato wa viongozi wangu kunitafutia nyumba ya kuishi,” anasema.

KUREJEA TANZANIA KULIMPA SOMO

Anasema baada ya kuvunja mkataba na Al Jahra ya Kuwait na kuamua kurejea Tanzania, amekutana na changamoto ambazo hakuzitarajia hivyo anaahidi kuwa hatarajii kupoteza fursa aliyoipata kwa mara nyingine.

“Niliporejea nyumbani, timu nyingi zilinihitaji zikiwemo kongwe, lakini yakatokea mambo mengi nikaamua kujiunga na Namungo FC ambayo nashukuru walikaa na mimi kwa kuniamini ingawa sikuwa na msimu mzuri sana,” anasema.

Anasema alijifunza kutofautisha soka la nje na nyumbani, jambo litakalompa muongozo katika majukumu yake na timu yake mpya hapo JS Saoura.

“Kiukweli kuna wachezaji wanaopambana nje kama kaka yangu Mbwana Samatta na Simon Msuva wanastahili heshima kwa kile wanachokifanya.”

“Baada ya kucheza nje na kugundua namna timu za mataifa ya wenzetu yanavyothamini mchezaji, niliporudi Tanzania nimegundua kuwa nafasi niliyoipata sasa sio ya kuchezea natakiwa kupambana ili niweze kufikia malengo,” anasema Salamba.