Wakati jopo la wataalamu wakindelea kuchakata CV za makocha waliotuma maombi ya kuajiriwa kuwa Kocha Mkuu wa Simba, Kocha wa zamani wa wekundu wa msimbazi, Mbeligiji Patrick Aussems amejitosa rasmi kuomba kukinoa kikosi hiko.
Aussems ambaye alifanikiwa kuipeleka Simba robo fainali ya Klabu Bingwa msimu wa 2018/ 19 amejitosa kuomba nafasi hiyo huku kukiwa na joto kali la nani atarithi mikoba ya Mfaransa Didier Gomes ambaye kibarua chake kimesitishwa.
Chanzo kutoka Simba SC, Kimeiambia Soka la Bongo kuwa, Aussems pamoja na kuwa aliondoka Simba kwa kuwakashifu mabosi kadhaa wa Klabu hiyo, bado ananafasi kubwa ya kurudishwa na kupewa kibarua hiko.
“Mchakato ni mgumu, kuna makocha wengi sana wenye CV kubwa na ndogo wametuma maombi yao kuomba ajira hii, lakini pia yupo Patrick Aussems, japo kuwa aliondoka hapa kwa kuwakashifu wajumbe wa Bodi pengine anaweza kufikiriwa haswa ukizingatia kuwa alifanya kazi nzuri” Chanzo cha taarifa hiyo kwa Soka la Bongo.
Itakumbukwa kuwa akiwa na Simba, Aussems aifanikiwa kuifanya timu hiyo icheze soka la wazi na kushambulia muda wote hali iliyopelekea kuifanya timu hiyo kufuzu hatua ya makundi Ligi ya mabingwa msimu wa 2018/19 na hatimaye robo fainali ambapo walitolewa na TP Mazembe.
Mara baada ya kufukuzwa Simba, Aussems alinukuliwa kuwa Klabu hiyo inaongozwa na watu washamba na wasio soma, huku taarifa za ndani kutoka klabuni hapo zikidai kuwa kocha huyo alishindwa kuwa muangalizi mzuri wa wachezaji , ambapo alishutumiwa kujihusisha na ulevi uliopitiliza pamoja na kubariki matendo ya utovu wa nidhamu kwa baadhi ya wachezaji waandamizi.
Hivi sasa Aussesm ni Kocha Mkuu wa FC Leopards ya nchini Kenya, ambapo taarifa kutoka huko zinasema kuwa anapitia kipindi kigumu baada ya timu hiyo kuzuiwa kufanya usajili wa wachezaji wapya, huku wachezaji waliokuwepo wakiondoka karibu wote hivyo kujikuta akiwatumia wachezaji wa kikosi cha vijana.