Baada ya kucheza mechi nne mfululizo bila kuonja ushindi, leo Jumatano, Novemba 3, Tanzania Prisons itakuwa uwanjani tena kuwakabili Coastal Union huku kila timu ikihitaji pointi tatu za kwanza kwenye Ligi.
Hadi sasa Prisons ndio wanaburuza mkia kwa pointi moja, huku ikiwa miongoni mwa timu mbili zilizoruhusu idadi kubwa ya mabao (sita) sambamba na KMC.
Timu hiyo ya Jijini Mbeya inawakabili Wagosi wa Kaya ikikumbuka kipigo kizito cha mabao 3-0 ilichopata nyumbani kwenye uwanja wa Nelson Mandela mkoani Rukwa dhidi ya Biashara United, huku Coastal Union wakiambulia suluhu mbele ya Simba ikiwa ni sare ya tatu kwao na kupoteza mechi moja.
Mchezo huo ambao utapigwa Mkwakwani Jijini Tanga, unatazamwa kuwa na ushindani katika vita ya pointi tatu ili kujinasua nafasi za chini katika msimamo wa Ligi Kuu.
Mbali na mchezo huo, utakaopigwa saa 8 mchana, mbungi nyingine itazikutanisha Biashara United dhidi ya Mbeya City mechi itakayopigwa uwanja wa Kumbukumbu ya Karume mjini Musoma.
Mchezo huo wa raundi ya tano, utakuwa na mvuto zaidi kutokana na timu zote kuhitaji alama tatu na kupanda nafasi za juu, ambapo hadi sasa Mbeya City wapo nafasi ya saba kwa pointi sita, huku wenyeji wakiwa na alama tano nafasi ya tisa.