LIGI Kuu Bara imesimama kwa muda ili kupisha mechi za kimataifa kwa timu za taifa zinazoendana na kalenda ya Shirikisho la Soka Duniani (Fifa).
Hata hivyo, tayari mechi 40 zimeshapigwa ndani ya raundi tano za ligi hiyo, huku ikishuhudiwa zikitolewa kadi nyekundu nane hadi sasa, ilhali zikipigwa penalti tisa.
Kwenye ishu za kadi nyekundu kuna wachezaji wanne wamejikuta wakilimwa kadi hizo dhidi ya Simba, kuonyesha kwamba ukijichanganya kwa watetezi hao, basi ujue kabisa inakula kwako.
Katika mechi nne kati ya tano ilizocheza Simba zimewagharimu wapinzani wao kulambwa kadi nyekundu, licha ya kwamba hata wao walipata hasara kwenye mchezo mmoja kwa kumpoteza beki wa kati, Hennock Inonga ‘Varane’.
Usichokijua ni kwamba ni mchezo mmoja pekee uliokuwa wa kufungulia msimu ndio ambao Simba ilicheza bila kushuhudiwa akitolewa mchezaji kwa kadi nyekundu, lakini ilipata penalti ambayo ilipotezwa na nahodha John Bocco.
Tuachane na ishu za penalti ambapo Simba imefanikiwa kupata mara mbili katika mechi tano za awali za msimu huu, ikifunga nyingine kupitia Rally Bwalya, hapa chini ni rekodi za wachezaji watano waliojikuta wakishindwa kumaliza mechi dhidi ya Simba.
DODOMA JIJI v SIMBA
Mchezo huo ulipigwa katika Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma, huku Simba ikiibuka na ushindi wa bao 1-0 lililotiwa kimiani na Meddie Kagere dakika ya 70.
Anuary Jabir alilimwa kadi nyekundu dakika ya 44 katika mchezo huo baada ya kumchezea madhambi Kennedy Juma wakiwa katika harakati za kurukia mpira alipompiga kiwiko usoni.
Ilimpa wakati mgumu mwamuzi wa mchezo, Joackim Akamba kutoa uamuzi kwa wakati mpaka mwamuzi msaidizi alipoingilia kati, huku akisaidiwa na wachezaji wa Simba walioenda kumchomea Jabir alichofanya.
SIMBA v POLISI TANZANIA
Dakika ya 86 Juma Ramadhan alilimwa kadi nyekundu ikiwa ni ya pili ya njano baada ya kumchezea madhambi Bernard Morrison katika harakati za kuokoa mpira na kunyanyua vibaya mguu ambao ulionekana kama umemgusa winga huyo Mghana aliyejiangusha.
Baada ya madhambi hayo ndani ya eneo la hatari dakika ya 89, mwamuzi Abel William kutoka Arusha aliamua kupigwa mkwaju wa penalti uliopigwa na Bwalya na kuwafanya Simba kupata pointi tatu kwa kushinda bao 1-0 na kumuacha kipa Metacha Mnata akiduwaa.
SIMBA v COASTAL UNION
Katika mchezo huo Simba ilitoka sare ya bila kufungana, huku kadi mbili nyekundu zikitolewa kwa pande zote mbili. Kadi ya Benedictor Mwamlangwa aliyomwa dakika ya 73 ikitanguliwa na njano iliyokuwa ya pili na kusindikizwa na nyekundu. Awali, alionywa kwa kadi ya njano dakika ya 17 na mwamuzi Rafael Ikambi kutoka Morogoro baada ya kumchezea madhambi Sadio Kanoute.
Hata hivyo, baadaye alimchezea faulo Inonga na wakati wa kutaka kupigwa friikikii aliupiga mpira akimzingua Inonga na kuishia kupewa kadi ya njano ya pili na nyekundu juu.
Wakati mashabiki wa Simba wakiamini mambo yameisha beki wao, Inonga alikumbana na umeme dakika ya 90 baada ya kumpiga kichwa Issa Abushehe aliyemvuta jezi wakati akitaka kupiga mpira wa faulo.
SIMBA v NAMUNGO
Katika mchezo huo ulioamuliwa na mwamuzi Nassoro Mwinchui, Simba ilishinda bao 1-0 lililofungwa na Kagere dakika tano za nyongeza, lakini wapinzani wao wakiwa pungufu.
Abdulaziz Makame alilimwa kadi nyekundu ya kujitakia baada ya kumchezea rafu Shomary Kapombe ambaye alilazimika kuruka juu kukwepa daruga la kiungo huyo aliyeonekana kudhamiria.
Makame alifanya ubishi kutoka, lakini baada ya kutuliza akili alibaini hakufanya sahihi na kumuomba radhi Kapombe na wadau wa soka kwa kitendo alichofanya uwanjani.