Home news HITIMANA: NIMEWATENGENEZA UPYA MKUDE NA AJIB…AFUNGUKA ALIVYOKATAA UKOCHA MKUU SIMBA…

HITIMANA: NIMEWATENGENEZA UPYA MKUDE NA AJIB…AFUNGUKA ALIVYOKATAA UKOCHA MKUU SIMBA…


KOCHA msaidizi wa Simba, Hitimana Thiery amekiri kwenye mahojiano maalum na Gazeti la  Mwanaspoti kwamba pamoja na vyeti alivyonavyo, ameingia kwenye timu hiyo ikiwa na presha kubwa sana ya matokeo lakini ameshazoea.

Lakini akaweka wazi kwamba amekaa na wachezaji wengi wazawa aliobaini kwamba na wana uwezo mkubwa na akawarudisha mchezoni kwa haraka akiwemo Ibrahimu Ajibu na Jonas Mkude. “Mfano mzuri nilivyowajenga Ibrahim Ajibu na Jonas Mkude, nilitumia hekima na busara, ili wanielewe namaanisha kitu gani juu ya hatma yao ya soka. Upole wangu haumaanishi ni mzembe kazini, nasimamia majukumu yangu ipasavyo, wakati mwingine nazungumza na wachezaji kama wadogo zangu, kuwaambia namna nyakati haziwezi kurudi nyuma, nilikuwa mchezaji kama wao na sasa ni kocha wao,” anasema.

“Siku ya kwanza nilivyokaa na Mkude na Ajibu niliwaambia ukocha nauweka pembeni, nakaa na nyie kama wadogo zangu, nikawaeleza nilikuwa mchezaji mkubwa niliyecheza timu kubwa kama wao, nyakati zikapita na sasa ni kocha wao, nao nyakati zao zitapita wanapaswa kumaliza kwa kuweka rekodi ya heshima.

“Unajua mchezaji ukimwambia ukweli unamjenga, niliwaambia hawataanza moja kwa moja kuingia kikosini baada ya kuzungumza nao, jinsi wanavyopaswa kuishi, kwani timu ilikuwa na presha kubwa, baada ya kuona upenyo niliwaambia watacheza dhidi ya Namungo FC wakacheza na watu wakaona walichokifanya,”anasema.

“Mashabiki wengi wanajiuliza mbona fulani hachezi, mfano Gadiel Michael, bado ligi ni mbichi, anakuja kocha mkuu, ajipange aonyeshe atapata nafasi ya kucheza kama wengine,” anasema.

WAWA BENCHI

Anasema baada ya kupigwa na Galaxy hakuna mtu ambaye alitegemea matokeo yale, jambo lililoleta presha kubwa katika mitaa na mitandao ya kijamii dhidi ya beki wao wa kati, Pascal Wawa.

“Kelele zile zilimuathiri Wawa, kocha ni kama baba, niliamua kumuweka mbali na kelele hizo na uzuri amenielewa, ila bado ligi ni ndefu, Wawa atarejea uwanjani na atacheza mechi nyingi zilizopo mbele yetu,” anasema kocha huyo wa zamani wa Namungo ambaye mashabiki wanajiuliza kwanini asingepewa ukocha mkuu?

APENDEKEZA KOCHA MKUU

Baada ya Didier Gomes kutimuliwa; “Kwa presha ambayo ilikuwepo, niliwaambia viongozi wangu wamtafute kocha mkuu ambaye tutakuwa chini yake, lengo ni kuhakikisha Simba inakuwa na muendelezo wa furaha ambayo walikuwa nayo miaka minne iliyopita,” anasema.

SOMA NA HII  MPOLE: "SIMBA IANGALIWE KWA JICHO JINGINE...UBORA WA SIMBA UMEIFANYA YANGA KUJITAFAKARI

“Nimejiunga Simba kwenye nyakati ngumu, mtu anaweza akajiuliza nina Leseni A niliyosomea Ujerumani kwa nini sikuendelea kuwa kocha mkuu, nilifanya maamuzi ya kushauri viongozi kwa faida ya Simba kuliko kutanguliza maslahi yangu binafsi, akija tutasaidiana naye.

“Ndio maana programu ninazofanya ni kuiweka miili tayari na kutengeneza ufiti kwa wachezaji, ili ya ufundi aje ayafanye kocha mkuu na programu zake na sisi tutakuwa tunafuata maelekezo yake,” anasema na kusisitiza kuwa hakupendekeza jina la kocha huyo wala hamfahamu.

“Pamoja na kwamba Ligi ya Mabingwa Afrika, nilikuwa nasimama mimi benchi, ukweli ni kwamba nilikuwa nafuata maelekezo ya Gomes, akiona kitu hakiendi sawa alikuwa anapiga simu na nilikuwa nafanya anachokitaka.

Kuhusu ujio wa Pablo Franco anasema; “Yule ni kocha mkuu, kazi yangu ni kumshauri, siwezi kumshawishi afanye ninachoona mimi, akija akawaona wachezaji, akiniuliza nitamshauri ila siyo kuanza kutengeneza mazingira fulani kabla ya kuniuliza, kitu nisichoweza kukifanya,” anasema Hitimana ambaye ana uzoefu mkubwa na soka la Afrika.

ALIPOACHIWA TIMU

Anakiri alikuwa kwenye presha kubwa, ambayo hajawahi kuipata katika maisha yake ya soka.

“Mashabiki walizoea raha, zikaja mechi mbili zilizowatoa mchezoni, hii haikuwa rahisi kwangu, japokuwa nilikuwa nazungumza na wachezaji, wakati mwingine nilikuwa namuita mmoja mmoja, lengo ni kuwajenga na kuwarejesha njia kuu,” anasema.

MAJUKUMU NA MATOLA

“Tulikuwa wasaidizi maana yake tuli-kuwa tunamsaidia majukumu Gomes, ndivyo ita-kavyoku-wa kwa kocha mkuu ajaye, programu zake ndizo tutakazokuwa tunazitendea kazi,” anasema kocha huyo huku akisisitiza kwamba amejifunza mambo mengi ndani ya muda mfupi.

GOMES AMVUTA SIMBA

“Baada ya Simba kuona nimekuja Mtibwa Sugar, kufanya nao kazi, wakanitafuta na kilichofanya dili lao likamilike bila shida nilikuwa sijasaini mkabata, hivyo nikawalipa gharama zao zote za kunileta Tanzania,”anasema Hitimana ambaye ni miongoni mwa makocha wanaokuja juu kwenye soka la Afrika Mashariki.

“Basi maisha yangu na Simba yalianzia hapo katika nafasi ya usaidizi chini ya Gomes ambaye alikuwa ananihitaji na CV yangu iliwashinda makocha wengine waliomba nafasi hiyo kwa wakati huo,” anasema Hitimana na kukiri kwamba walikuwa wanafamiana na Gomes kitambo hata kabla ya kuja kufundisha ndani ya Simba. 

Credit: Mwanaspoti