Kocha Mkuu wa Yanga Nesreddine Nabi amewapa mapumziko ya siku mbili wachezaji wake mara baada ya kurejea katika kambi fupi ya kisiwani Zanzibar.
Kocha Nabi amesema katika safari yao ya Zanzibar imekuwa ya mafanikio ambapo ameamua kuwapa mapumziko ya siku mbili wachezaji wake kisha warudi kazini Jumanne Novemba 16 kujiandaa na mchezo dhidi ya Namungo ugenini.
“Tulikuwa na wakati mzuri kule Zanzibar tumepata nafasi ya kupanga mambo yetu lakini kitu cha kufurahisha mashabiki nao wa kule wamefurahia ushindi wa timu yao,”amesema Nabi.
“Tutapumzika kwa siku mbili tuwape nafasi vijana nao kuona familia zao na baada ya hapo tutarudi kazini Jumanne kuendelea na maandalizi ya safari yetu.”
Nabi amesema anaamini wachezaji wake nane ambao wako katika majukumu ya timu za taifa watarejea kwa wakati na salama ili waanze maandalizi ya mwisho wakiwa pamoja wakiwafuata Namungo.
“Mechi ya Namungo ni ngumu kitu nakiomba hapa ni wachezaji wangu wote kurudi salama lakini pia warudi kwa wakati tunatakiwa kujipanga tukiwa kama kundi moja kabla ya mechi hizo mbili za ugenini.”
Wachezaji wa Yanga ambao wako katika timu za taifa ni Khalid Aucho (Uganda), kipa Diarra Djigui (Mali), Ramadhan Kabwili, Kibwana Shomari, Dickson Job, Bakari Mwamnyeto, Zawadi Mauya, Feisal Salum (wote Tanzania) na Djuma Shaban (DR Congo).