Home news KAMWAGA: SIMBA NA PABLO FRANCO; HATUA MOJA TU LAKINI HATUA KUBWA SANA…

KAMWAGA: SIMBA NA PABLO FRANCO; HATUA MOJA TU LAKINI HATUA KUBWA SANA…


Julai 20 mwaka 1969, dunia ilimshuhudia mwanaanga Neil Armstrong akikanyaga mwezi kwa mara ya kwanza. Maneno yake mashuhuri wakati ule wakati aliposhuka kwenye chombo cha angani na kukanyaga mwezi yalikuwa haya; “That’s one small step for man. One giant leap for mankind.”

Alimaanisha hatua yake ile kutoka kwenye chombo kukanyaga mwezi ni hatua moja tu ya kawaida lakini kitendo cha hatua yake kama mwanadamu kukanyaga mwezi ni hatua kubwa mno kwa ubinadamu. 

Hakuna aliyedhani kwamba kuna siku mwanadamu atakanyaga mwezini. Angefikaje? Mwanadamu huyu asiye na mabawa angefikaje kwenye mwezi? 

Na wapo walioamini kwamba huko mwezini kufika ni kujitakia kifo tu. Kufika mwezini ilikuwa ni hatua ya kipekee sana. 

Ndiyo naweza kutoa maelezo hayo kuhusu ujio wa Kocha Pablo Franco kutoka Hispania kuja Simba SC. 

Yeye ni kocha tu kama walivyo makocha wengine waliowahi kufundisha Simba. Labda naye atafundisha na siku moja atafukuzwa kama wengine. 

Lakini, jambo kubwa moja hapa ni moja; kwamba leo klabu kutoka Tanzania inasajili kocha aliyewahi kufundisha kwenye Ligi Kuu ya Hispania. 

Ligi ya Cristiano Ronaldo na Lionel Messi. Ligi ya Jose Mourinho na Pep Guardiola. Ligi ya Xavi na Iniesta!!! 

Let that sink in!!! Pumua kidogo. 

Kwa Tanzania, Simba ni timu kubwa. Lakini katika uwanda mpana wa soka duniani, Simba ni wadogo. Hatuwezi kuzungumzwa kwenye level moja hata na Al Ahly tu ya Misri achilia mbali huko nje. 

Binadamu mwenda mwezini hajapata kitu cha maana kule. Hajaokota madini. Hajaokota fedha nyingi. Lakini lengo moja lilitimia – kwamba mwanadamu akiweka nguvu zake kwenye kitu lolote linawezekana. 

Hilo sasa ndilo uongozi wa sasa wa Simba umeonyesha kwa washabiki wake na jumuiya ya soka duniani. Kwamba lolote linawezekana. Ukitaka jambo kwa jitihada na maarifa utalipata.

Simba itapata nini? 

Simba inapata mwalimu wa daraja la juu kabisa mwenye uwezo wa kufundisha popote duniani. Kama atakaa hata kwa kipindi kifupi, kuna kitu atakiacha kwa wale waliofanya naye karibu. 

Kocha mmoja anaweza kuwa na ushawishi mkubwa kwenye mnyororo mzima wa thamani wa mchezo. 

Chukulia mtu kama Pep Guardia. Uingereza leo wanasema aina yake ya uchezaji ndiyo sasa inafundishwa hadi na makocha wa watoto England nzima. 

Alipokuwa Hispania, taifa hilo lilitwaa Kombe la Dunia. Alipokuwa Ujerumani, walitwaa Kombe la Dunia. England almanusura itwae Kombe la Ulaya mwaka jana na watu wanaitazama kitofauti kwenye Kombe la Dunia nchini Qatar mwakani. 

SOMA NA HII  KIPA WA YANGA AGOMBEWA NA TIMU KIBAO ZINAZOSAKA SAINI YAKE

Si lazima Pablo awe na mchango wa namna hiyo kwa Tanzania lakini nilitaka kujenga mfano wa namna mtu mmoja anavyoweza kubadili mfumo mzima wa soka kwa uwezo wake. 

Kama wachezaji wa Simba wakiwa na kiwango kizuri – maana yake Taifa Stars itanufaika. Katika historia ya soka ya taifa letu, Tanzania inakuwa na timu ya taifa yenye mafanikio wakati Simba inapokuwa nzuri. Cheki tu kwenye historia yetu na utaona ukweli huu. 

Ujio huu wa Pablo umekuja wiki chache baada ya taarifa kwamba mitandao ya kijamii ya Simba SC inakua kwa kiwango cha kufananishwa na timu kama Manchester United. 

Sevilla ilikuja Tanzania miaka michache iliyopita na si kama mabadiliko kwenye timu yaliyofanywa na kocha Patrick Aussems, Wahispania wale walikuwa wanapigwa hapa. 

Hoja yangu ni kwamba daraja, heshima na hadhi ya Simba inazidi kupanda na mawazo yanazidi kuwa makubwa. Wanachama nao sasa wanaanza kuwa na ndoto kubwa. 

Ni jambo kubwa sana ambalo Mwenyekiti wa Bodi, Salim Abdallah Mhene na Ofisa Mtendaji Mkuu, Barbara Gonzalez – pamoja na wakurugenzi wengine wa klabu, wamelifanya kwenye kumleta kocha wa hadhi hii. 

Ikitokea nafasi ya kocha wa Simba ikawa wazi tena, makocha watakaoitaka watakuwa wakubwa zaidi na bila shaka washindani wengine kwenye soka letu nao watataka kufikia viwango vya Simba. 

Kufikia viwango vya Simba na kupeleka soka letu kwenye  viwango vya juu mno. Viwango ambavyo wengine wanashangaa. 

Wanajiuliza; timu gani hii ya Tanzania inayoweza kumwajiri Pablo? Ina nini hiyo timu na viongozi na washabiki wake ni wa aina gani. 

Msishangae kuona tamaa ya kui follow Simba inaanza kuongezeka kwingineko. Na tamaa hiyo ndiyo sasa itatengeneza biashara nyingine ambayo hadi sasa hatuwezi kuiona kwa macho yetu. 

Watu wengine watamjadili kocha huyu kwa takwimu zake. Watamjadili kwa mwonekano wake. Watamjadili kwa nafasi alizoshika huko nyuma. 

Jambo moja ambalo haliwezi kuelezwa ni namna ambavyo Simba imevunja ile glasi ya kioo ( a glass ceiling) kwa kumleta mwalimu wa kaliba ambayo hajawahi kuletwa kwenye Ukanda wetu huu wa soka. 

Hatua ile ya Pablo Franco kutua kutoka kwenye ndege iliyomleta na kukanyaga ardhi ya kawaida ni hatua ya kawaida sana kwa mtu yeyote. Ni hatua moja tu.

Lakini kwa kocha wa aina yake kujiunga na Simba, hiyo ni hatua kubwa, kubwa sana kwa klabu na kwa soka la nchi yetu. 

Ezekiel Kamwaga

London

England.