HERITIER Makambo, mshambuliaji wa Yanga mambo yanaonekana kuwa magumu kwakwe kwenye upande wa kucheka na nyavu katika mechi za mashindano kwa kuwa amekwama kufunga katika mechi tano za mashindano.
Kwa msimu wa 2021/22, Yanga inayonolewa na Kocha Mkuu, Nasreddine Nabi imecheza jumla ya mechi 7 za mashindano ya ndani huku Makambo akicheza katika mechi tano na kutumia dakika 149 bila kufunga.
Nyota huyo ambaye amerejea Yanga akitokea kikosi cha Horoya ya Guinea alianza kuyeyusha dakika katika mchezo wa Ngao ya Jamii mbele ya Simba, Septemba 25 alitumia dakika 21 timu yake ilishinda bao 1-0 na mtupiaji alikuwa ni Fiston Mayele kwa pasi ya Farid Mussa.
Septemba 29 ilikuwa ni mchezo wake wa kwanza wa ligi ambapo alitumia dakika 28 mbele ya Kagera Sugar na Yanga ilishinda bao 1-0 na mtupiaji alikuwa ni Feisal Salum.
Oktoba 2 ilikuwa Uwanja wa Mkapa, Yanga ilishinda bao 1-0 dhidi ya Geita Gold alitumia dakika 26 mtupiaji alikuwa ni Jesus Moloko kwa pasi ya Yacouba Songne.
Oktoba 19 ilikuwa ni Uwanja wa Majimaji, Songea alitumia dakika 66 mbele ya KMC na ubao ulisoma KMC 0-2 Yanga mabao yalifungwa na Feisal pamoja na Mayele hawa kila mmoja alimpa pasi mwenzake.
Oktoba 30 mbele ya Azam FC hakuweza kupata nafasi ya kucheza ila Yanga ilishinda mabao 2-0,Novemba 2 mbele ya Ruvu Shooting hakupata nafasi ya kucheza lakini Yanga ilishinda mabao 3-1 na mchezo wa mwisho ilikuwa mbele ya Namungo 1-1 Uwanja wa Ilulu alitumia dakia 8 na mtupiaji alikuwa ni Said Ntibanzokiza.
Katika mabao 11 ambayo Yanga imefunga hajahusika katika bao lolote na nafasi yake ikiwa ni ushambuliaji.Kwa mujibu wa Mwinyi Zahera, Mkurugenzi wa Ufundi kwenye kikosi cha Vijana Yanga aliliambia Championi Jumatatu kuwa mchezaji huyo amekosa hali ya kujiamini.
“Makambo ni mchezaji mzuri ila kwa sasa amekosa ile hali ya kujiamini kwa kuwa hajapata muda mrefu wa kucheza na kufunga, akifanikiwa kufunga atarejea katika hali ya kujiamini ninamjua ni mchezaji mzuri,” .