Benchi la Ufundi la Mabingwa Watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara Simba SC linatarajia kufanya mabadiliko kwenye kikosi kitakachoshuka dimbani leo Jumatano (Desemba Mosi).
Simba SC itakuwa mwenyeji wa Geita Gold katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam, kwenye mchezo wa mzunguuko wa saba wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Kocha Msaidizi wa Simba SC Seleman Matola amezungumza katika Mkutano na Waandishi wa Habari jana Jumanne (Novemba Mosi) jijini Dar es salaam, ambapo amesema maandalizi ya kikosi chao yamekamilika na wanakwenda kupambana na Geita Gold wakiwa na lengo la kuzipata alama tatu muhimu.
Hata hivyo Matola amesema kutakua na mabadiliko kwenye kikosi cha Simba SC, ambapo baadhi ya wachezaji wanatarajiwa kupumzishwa kwa ajili ya mchezo wa mkondo wa pili wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Red Arrows ya Zambia.
“Kesho kutakuwa na baadhi ya mabadiliko sababu ya kujiandaa na mchezo wa marudiano wa Kombe la Shirikisho Afrika, lakini la kufurahisha wachezaji wote wako vizuri na yeyote anaweza kuanza na kuleta matokeo.” amesema Matola
Baada ya mchezo wa leo dhidi ya Geita Gold, Simba SC itaanza maandalzii ya mchezo wa Mkondo wa pili wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Red Arrows, ambao utapigwa mjini Lusaka Jumapili (Desemba 05).
Katika mchezo wa Mkondo wa Kwanza wa Kombe la Shirikisho Afrika Simba SC, iliibuka na ushindi wa mabao 3-0, Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.